2016-10-31 16:25:00

Jiandaeni kushangazwa na miujiza ya upendo na huruma ya Mungu!


Askofu mkuu Antje Jackelèn mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri nchini Sweden pamoja na Askofu Anders Arborelius wa Jimbo Katoliki la Stockholm wameshirikisha sala na maombi yao kwa Mwenyezi Mungu wakati wa Ibada ya kiekumene kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani kwenye Kanisa kuu la Lund, Jumatatu, tarehe 30 Oktoba 2016. Askofu mkuu Antje Jackekèn amewataka wakristo kuwa na ujasiri wa kuangalina uso kwa uso, ili kushirikishana maajabu ya Mungu na wasi wasi inayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo; tayari kushangazwa na miujiza ya upendo na huruma ya Mungu, ili kufurahia uwepo wa Kristo kati yao.

Wakristo wanasikitishwa kutokana na hatari zinazosababishwa na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote pamoja na jamii nyingi kuendelea kumeguka kutokana na chuki na uhasama pamoja na kupoteza wenzi wao. Wanasikitishwa, lakini wanasherehekea zawadi ya uhai. Wanaendelea kusikitishwa kutokana na mipasuko ya familia ya binadamu, lakini, wanamshukuru Mungu kwamba, Wakristo wameanza mchakato wa kutoka kwenye kinzani kuelekea kwenye umoja, hali inayohitaji waamini kubadili mawazo, mioyo na mtindo wao wa maisha, ili kutenda katika matumaini. Wakristo wanasherehekea matumaini ya imani, toba na nguvu ya Mungu inayokoa na kuponya; ili kweli: haki, amani na matumaini yaweze kutawala!

Askofu Anders Arborelius wa Jimbo Katoliki la Stockholm amewakumbusha Wakristo kwamba, Kristo Yesu kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, aliwaombea wafuasi wake kuwa na umoja unaopata chimbuko lake kutoka  kwenye Sakramenti ya Ubatizo. Wakristo wanasikitishwa kutokana na dhambi pamoja na mapungufu yao ya kibinadamu yaliyosababisha utengano. Ni matumaini na ndiyo sala yao kwamba, waweze kuwa na umoja kamili, unaoonekana utakaokuwa ni ushuhuda kwamba, Kristo Yesu amefufuka kweli kweli na yuko kati yao na anatenda pamoja nao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.