2016-10-31 16:08:00

Historia ni Nabii anayetaza mbali kwa matumaini!


Katibu mkuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kilutheri Duniani, Daktari Martin Junge, katika mahubiri yake wakati wa sala ya Kiekumene kwenye Kanisa kuu la kilutheri Lund, nchini Sweden, katoa mwaliko kwa wajumbe na wanaharakati wote wa Uekumene, kuwa matawi yenye uhai kwa kubaki katika misingi ya mti wa Uzima, ambao ni Yesu Kristu mwenyewe, Uzima wa kweli, kwani kujitenga na mti huo, matawi hayo hayawezi kuzaa matunda.

Dr. Martin Junge amewakumbusha wajumbe kuwa kumekuwako wanawake na wanamume wengi ambao umoja wao katika kuhangaikia Umoja wa Wakristo umekuwa mfano wa kuigwa. Kwa Nyakati mbali mbali wamekuwa wakijikusanya kuombea umoja au kupambana katika kujenga jumuiya za kiekumene. Wamekuwako Wanataalimungu walioingia majadiliano ili kuzishinda tofauti za Mafundisho dini na taalimungu kati yao; na wamekuwako watumishi waliojikita katika kuhudumia maskini na wanaoonewa; na pamoja nao ni wale waliotoa uhai wao kwa ajili ya Injili, wakafa mashahidi. Kasema Dr. Martin kuwa: anasukumwa kutoa shukrani za dhati kwa manabii kama hao waliotangulia.

Kaalika kudumisha na kuongeza juhudi za kuishi katika Jumuiya na kutoa ushuhuda wa pamoja, ambazo ni ishara za kuishi kama matawi yaliyo pamoja katika mti wa Uzima, na sio matawi yaliyotawanyika na kukosa uhai. Kwa namna hii Yesu Kristo, mti wa Uzima, ataweza kutambuliwa kati ya watu wenye kuteseka na kuonewa, na wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Vinginevyo watajitenga na Kristo aliye Uzima wa kweli, iwapo wataendekeza mafarakano na chuki.

Iwapo Kristo ataonekana kati ya watu na jumuiya zote bila kujali tofauti zao, ndivyo wanadamu na jumuiya mbali mbali zitaanza kutazamana kwa namna nyingine, namna ambayo itafungua macho na kugundua kuwa Wakristo wana mambo mengi zaidi yanayowaunganisha, kuliko yanayowatenganisha au kuwatofautisha, sababu wote ni matawi ya mti mmoja wa Uzima, wote ni wamoja katika Ubatizo mmoja. Na ni dhahiri, kwani ndiyo sababu wanakutana katika sala na mazungumzano, ili kuvumbua zaidi kuwa wote ni mali ya Kristo, na wote wamo ndani ya Kristo.

Tangu mwanzo wa ufunuo huo wa umoja walio nao ndani ya Kristo, kumekuwa na udhaifu pia wa kugawanyika kwa Kanisa hilo moja, ambalo ni Mwili wa Kristo. Katika mtazamo wa umoja uliojengeka ndani Kristo, pamoja na uzuri na matumaini yote yanayowahamasisha, kuna maumivu makali pia ya madonda ya ugawanyikaji kati ya Makanisa. Ikiwa watauvunja umoja, watakuwa wamevunja na kupoteza zawadi waliyopewa na Kristo, na hakuna sababu yeyote ya kuwafanya wauvunje umoja wao, amesisitiza Dr. Martin Junge.

Amewaalika wote kutafakari ni kwa namna gani wanaweza kuendelea kutembea kwa pamoja kwa juhudi, ujasiri na matumaini yale yale waliyoanza nayo watangulizi wao, katika hija hiyo ya kiekumene ndani ya umoja!; namna gani wanaweza kutembea kwa bidii kuelekea ule umoja wa jumuiya ya Kikristo ambayo wanaitiwa na Mungu mwenyewe!; kuona namna gani mwishowe wanaweza kuponya madonda ya mgawanyiko na kufikia kuwa kweli matawi ya mti mmoja wa Uzima ndani ya Kristo!

Dr. Martin Junge, kamnukuu mwandishi mmoja wa Marekani ya Kusini, Bwana Eduardo Galeano, aliyewahi kuandika kwamba: historia ni nabii anayetazama mbali, kwa kile alichokuwa, dhidi ya kile alichokuwa na kutangaza kile atakachokua. Kawaalika kwa namna hiyo, wajumbe wa Kiekumene, kuanzia sasa kuchukua ujumbe huo kama ufunguo wa kusoma na kutafakari ujumbe wa Maandiko Mtatakifu, juu ya Uzima wa kweli. Kwamba ujumbe na namna hiyo ya mtazamo, viwe habari njema ya matumaini na unabii wa umoja madhubuti wa maisha, na kuzaa matunda ya afya na uzima kamili. Hii iwe ndiyo roho ya kukutanika kwa pamoja na kuchukuliana kati ya Wakatoliki na Walutheri, waishinde ile historia iliyotiwa doa kwa mgawanyiko na marumbano, na kuelekea katika umoja zaidi.

Safari hiyo kuelekea umoja, itawahitaji watu binafsi na jumuiya mbali mbali kuweka juhudi katika mazungumzano ya kina, na kuepuka kung’ang’ana na tofauti kati yao, ingawa kumbukumbu zao zina doa la mgawanyiko na marumbano. Hivyo waweke kwa pamoja zile nguvu za kutafuta umoja, wawe manabii wa matumaini, uponyaji wa kweli, ili kwa pamoja wawe tumaini kwa mwanadamu. Tumaini la dunia ya amani, haki na upatanisho. Ambavyo kwa sasa ni fumbo kubwa na la kina kwa mwanadamu.

Kuna Jumuiya mbali mbali na watu binafsi, wanaoishi kwa mateso, katika machafuko na uonevu, wanatoa kilio chao wakihitaji msaada, naye Mungu anasema na Wakristo kwa kuwasisitiza masikioni mwao kupitia Neno Lake, wajibu kilio hicho wakiwa katika umoja, na ndani ya mti mmoja wa Uzima, Yesu Kristo. Wanaalikwa kuzaa matunda ya amani, haki, upatanisho, huruma na mshikamano. Dr. Martin amewaalika wajumbe, kuvunja kuta za mgawanyiko na waitikie wito wa Kristo kuwa Mabalozi wa Upatanisho. Mungu anataka awatumie kujenga madaraja kati ya watu, kujenga Nyumba yakukutana kwa pamoja, na Meza ya kushiriki Mkate na Mvinyo kwa pamoja.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.    

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.