2016-10-30 10:21:00

Yale ambayo Wakristo wanapaswa kujifunza kutoka kwa Martin Luther!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni tarehe 29 Oktoba 2016 alikwenda kusali na kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya warumi, wakati huu anapojiandaa kuanza hija yake ya kitume nchini Sweden kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi tarehe 1 Novemba 2016 kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumsindikiza kwa sala, ili aweze kuwa kweli ni chombo na shuhuda wa umoja wa Wakristo!

Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Umoja wa Wakristo anasema, Ukuu wa Mungu na utangazaji wa Injili ya Kristo ni kati ya mambo makubwa ambayo Martin Luther ameacha kama urithi wake katika maisha ya kiroho kwa Wakristo. Utajiri huu unapaswa kufanyiwa kazi na Wakristo wote ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano katika mambo matakatifu. Viongozi wa Mageuzi ya Kiluteri Duniani hawakuwa na nia ya kulivuruga Kanisa la Kristo na hatimaye, kuanzisha Makanisa mengine kama ilivyojitokeza baadaye, lakini jambo la msingi lilikuwa ni namna bora zaidi ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa mataifa.

Inasikitisha kuona kwamba, historia, ikachukua mkondo tofauti kabisa na ule uliokuwa umelengwa na watu kama Martin Luther. Huo ukawa ni mwanzo wa mpasuko wa Kanisa, vita vya kidini na kinzani za kijamii, kisiasa na kiuchumi na athari zake bado zinaendelea kusikika katika maisha ya watu wengi duniani. Kardinali Kurt Koch anasema, Kanisa Katoliki pia linabeba lawama katika hali zote hizi, kwani halikuwa tayari kukubali cheche za mageuzi zilizokuwa zinatangazwa na Martin Luther.

Kati ya mwaka 1522 hadi 1523 Papa Adriano VI aliomba msamaha kutokana na mapungufu yaliyojitokeza kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican na hivyo kushindwa kutoa maamuzi ya haki kwa Martin Luther. Kumbe, miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani ni kipindi cha kufanya kumbu kumbu badala ya kusherehea. Maadhimisho haya kwa mwaka huu, anasema Kardinali Kurt Koch yanachukua mwelekeo wa pekee, unaojikita katika majadiliano ya kiekumene katika toba na wongofu wa ndani, ili kuambata zaidi yale yanayowaunganisha Wakristo badala ya kuendekeza kinzani na mipasuko ya Kanisa iliyojitokeza miaka iliyopita.

Baba Mtakatifu anakazia Uekumene wa: Sala, maisha ya kiroho, huduma na ushuhuda wa damu ya mashuhuda wa imani wanaoendelea kuteseka sehemu mbali mbali za dunia, lakini zaidi huko Mashariki ya Kati, Ukanda ambao umegeuka kuwa ni Ukanda wa mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake! Ikumbukwe kwamba, wazo la kuadhimisha Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri kati ya Wakatoliki na Waluteri lilitolewa na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani na kuridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko.

Hiki ni kielelezo cha upendo, udugu na mshikamano katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayosimiwa katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo! Hakuna Kanisa ambalo ni maskini kabisa kiasi hata cha kushindwa kuchangia katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na umoja wa Kanisa anasema Kardinali Kurt Koch. Wala hakuna Kanisa linaloweza kujidai kwamba, linajitosheleza kiasi hata cha kushindwa kupokea karama na utajiri kutoka kwa Makanisa mengine duniani. Makanisa yote yanapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo na imani kwa Kristo na Kanisa lake. Changamoto iliyoko mbeleni kwa Makanisa haya kwa sasa ni ni: Kanisa, Fumbo la Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu; tema ambazo bado ni tete sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Lakini, Wakristo watambue kwamba, kiongozi mkuu wa majadiliano ya kiekumene ni Roho Mtakatifu, hivyo wanapaswa kumwachia nafasi ili awaongoze katika hija ya umoja wa Kanisa kwa wakati muafaka!

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.