2016-10-30 09:17:00

Ukuu na heshima ya mtu vinajengwa na sadaka na majitoleo yake!


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican utakumbukwa kwamba, Jack Higgens ni mwandishi wa riwaya ‘The Eagle Has Landed’ – ‘Tai Ametua’ – aliulizwa ni kitu gani alipendelea kukijua au kukifahamu alipokuwa bado kijana. Jibu likawa, laiti ningejua kwamba ukifika juu, hakuna lo lote pale. Naye mwandishi R. H. Benson anasema kuwa – ukuu wa maisha ya mtu haupo katika sifa zake mbalimbali za nje bali katika majitoleo na sadaka zake.

Ndugu wapendwa, tunaona katika somo letu la Injili kuwa katika watu waliokuwa na mafanikio katika mazingira ya wakati wake ni huyu Zakayo ambaye leo tunasikia habari yake katika Injili takatifu. Kama mtoza ushuru alikuwa kibaraka wa watawala wapagani Warumi. Watoza ushuru walifanya kazi kwa niaba ya hawa watawala. Kwa hiyo walichukiwa kama vibaraka wa wapagani Warumi ambao hawakupendwa na Wayahudi na pia walichukiwa kwa kuwa kodi ilichukiwa na wenyeji. Mbele ya wenyeji walikuwa ni watenda dhambi. Huyu Zakayo alikuwa mtoza ushuru mkuu wa mji wa Yeriko. Kwa kawaida utawala uliweka kiwango cha kodi cha kutoa kwa mwaka lakini mtoza ushuru mkuu alikuwa na uwezo wa kuongeza kiwango ili abaki na kiasi kikubwa.

Kiuchumi na kijamii alikuwa na hali nzuri sana. Ila mbele ya watu wake alikuwa mtenda dhambi mkubwa. Huyu alisikia kuwa Yesu anapita mtaani kwao na alipenda kumwona. Huyu alivutwa na Yesu. Kwa kuwa alikuwa hapendwi na watu, ni mtu tajiri na maarufu alitafuta namna ya kumwona Yesu bila kuonekana na watu anaowatesa kwa kuwadai kodi. Aliazimia kupanda juu mtini na kujificha. Hata hivyo halikuwa chaguo zuri kwani kwa hadhi yake kupanda mtini kulimshushia hadhi zaidi. Yeye hakujali hayo ila kumwona tu Yesu. Hata hivyo Yesu alimwona na kumwita ashuke chini na kutaka kwenda nyumbani kwake. Na huo ukawa ndio wokovu wake.

Huu ukawa mwanzo mpya wa maisha yake. Ungamo la hali yake linamfanya ampate Yesu. Wengi wetu hatufikii hali hii ya ungamo au kujitambua na hivyo inakuwa vigumu kufanya mabadiliko. Zakayo ambaye alihukumiwa kuwa mdhambi anasema nusu ya mali yangu nawapa maskini na kama nimenyang’anya mtu kwa hila nitarudisha mara nne.

Huyu Zakayo anafanya sikitiko juu ya dhambi zake na anaweka nia ya kujisahihisha. Anakiri na kukubali ubaya aliotenda na anaweka nia ya kutotaka kufanya tena ule udhalimu.

Ndugu zangu, kama Zakayo hatuna budi kujitafakari sana juu ya hali ya maisha yetu ya kimwili, kiroho, kijamii n.k. Baada ya kusikia sehemu hii ya injili hatuna budi kuangalia na kuchunguza mazingira ya kazi zetu na nyajibu zetu mbalimbali. Ni nini tija yake? Mbele ya Mungu, watu na jamii inatazamwaje? Ipo hatari ya kuzama katika mahangaiko au majukumu yetu ya maisha na kutotambua watu wanasemaje au ni nini faida yake kwa jamii. Ni yapi matokeo ya kazi tuzifanyazo? Hivi kazi yangu ni ipi? Kuna falsafa moja ya kazi inasema ‘ kazi yako ni jina lako’. Je kazi yako au wajibu wako unatazamwaje na jamii? Wale unaowahudumia wanakuitaje au wanatambua hicho unachofanya?

Je uadilifu wetu katika kutimiza majukumu mbalimbali ukoje? Imekuwa lugha ya kawaida siku hizi kusikia habari juu ya ufisadi, rushwa, uvivu, ujambazi, wafanyakazi hewa, wanafunzi hewa, asilimia kumi, kupiga dili, mauaji ya albino na mambo kama hayo? Je sote au wenye dhamana ya uongozi tumekuwa wote kina Zakayo? Ni nani wanaofanya hayo yasiyofaa kwenye jamii? Ni wale? Wengine? Wao? Sisi je au mimi je nikoje? Je mimi, wewe, sisi ni Zakayo au Myahudi au Mrumi mtawala?

Jamii yetu inahangaika sana kujiweka vizuri kiuchumi, kimaadili, kiutawala n.k. Hakika inahitajika tafakari ya binafsi na hata ya kijamii. Tukoje? Tuko vizuri? Hatuna budi kuwa na ujasiri kama wa Zakayo. Pamoja na ukuu wake na hali yake katika jamii aliamua kujitokeza na Yesu akamwona na kumwita. Kwa lugha ya siku hizi alijiongeza na Yesu akamwona na kumwita. Hatuna budi sisi au wale wenye afadhali au waliokomaa kiimani wakaweza kuona wenye mahangaiko, kutambua waliko au wanayofanya na kunyoosha mkono wetu kuwaita. Hatuna budi kuwaona kama Yesu alivyomuona Zakayo juu mtini na kuita. Huu ndiyo uongofu unaohitajika kama alivyofanya Zakayo.

Mtu mmoja alinunua gazeti na kwa bahati mbaya katika ukurasa wa matangazo ya vifo uliandikwa wasifu wake ukiwa na kichwa ‘mfalme wa mabomu ya kutega ardhini afariki dunia’. Pamoja na kusikitika kwa taarifa hiyo iliyokosewa lakini akawa na hamu ya kujua mtazamo wa watu juu yake baada ya maisha yake hapa duniani. Kwa msisitizo taarifa iliandika na kusisitiza na kumtaja tajiri huyo kama ‘mfanya biashara wa kifo’. Ni kweli alivumbua mabomu ya kutega ardhini na alipata utajiri mkubwa kwa kuuza mabomu hayo. Kilichomshtua na kujiuliza ni  kuwa ni kweli alidhamiria kuwa mfanya biashara wa kifo? Kwa changamoto hiyo akapata kuongoka kutoka kuwa muuaji na kuwa mtu wa amani. Akaelekeza fedha zake, nguvu zake na mali yake katika kutafuta amani na kuborehsa maisha ya watu. Leo hii anakumbukwa si kama mfanya biashara wa kifo bali mtu wa amani na huyu ndiye mwanzilishi wa NOBEL PEACE PRIZE – ALFRED NOBEL.

Huu ndiyo uongofu unaohitajika kwa kila mmoja wetu. Leo tunaalikwa kufanya tafakari ya kazi zetu, wajibu wetu na majukumu yetu mbalimbali na kuona kama yana tija inayotakiwa. Kama tuonavyo hapo juu mwandishi R. H. Benson anavyosema ukuu wa maisha ya mtu haupo katika sifa zake mbalimbali za nje bali katika majitoleo na sadaka zake. Nasi pia hatuna budi kutoa sadaka za maisha yetu ili wengine wapate kuokoka.

Injili inaweka wazi tena leo “Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea”.

Tumsifu Yesu Kristo.

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.