2016-10-30 08:43:00

Makazi bora ni sehemu ya haki msingi za binadamu!


Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa katika mkutano wa makazi ya watu awamu ya tatu uliofanyika hivi karibuni mjini Quito, nchini Equador, amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na sera pamoja na mikakati itakayowawezesha watu wengi zaidi kuwa na makazi bora zaidi ili kuinua kiwango cha hali ya maisha. Hii inatokana na ukweli kwamba, makazi ni sehemu ya haki msingi za binadamu zinazotambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Leo hii, kuna makundi makubwa ya watu wasiokuwa na makazi maalum, wanaoishi katika makazi duni na hatarishi kwa utu na usalama wa maisha yao. Kuna sababu mbali mbali ambazo zinapelekea watu kukosa makazi bora na kudumu, lakini ikumbukwe kwamba, familia na makazi ni sawa na “uji kwa mgonjwa”, mambo ambayo kamwe hayawezi kutenganishwa. Serikali mbali mbali duniani hazina budi kuibua sera na mikakati ya ujenzi na maboresho ya makazi ya watu kwa kujikita katika kanuni auni, ili kweli haki msingi ya makazi iweze kutekelezwa, kama sehemu muhimu sana ya maendeleo ya watu.

Ardhi, Makazi na Ajira ni mambo msingi yanayofumbatwa katika mshikamano na kanuni auni, kwa ajili ya mafao ya wengi pamoja na ushiriki mkamilifu wa watu katika mchakato wa ujenzi wa demokrasia. Watu wajengewe uwezo wa kuwa na uhakika wa makazi bora, ili kulinda na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu na ukuaji wa familia. Katika mwelekeo kama huu, maskini pia wanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika sera za makazi ya watu.

Kutokana wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji, wazee na walemavu, wakati mwingine, Jumuiya ya Kimataifa inashindwa kuwapatia makazi bora na salama. Lakini, ikumbukwe daima kwamba, hata watu kama hawa wanatamani kuwa na makazi ya familia zao. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaendelea kuibua sera na mikakati kwa ajili ya ujenzi wa makazi bora ya watu, ili kulinda na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa maendeleo ya watu: kiroho na kimwili wakati alipokuwa anahutubia Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, New York, Marekani, mwezi Septemba, 2015 alikazia: ardhi, ajira na makazi ya watu kuwa ni vichocheo vya maendeleo ya watu sanjari na kukuza uhuru wa kuabudu, uhuru wa kupata elimu bora pamoja na haki nyingine za kiraia. Ili kufikia azma hii, kuna haja kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kanuni maadili kwa kupambana na rushwa, ukiritimba na tabia ya kushindwa kutekeleza maazimio yanayotolewa kwa ajili ya mafao ya wananchi wao.

Binadamu na mahitaji yake msingi, utu na heshima yake ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza badala ya sera na mikakati ya maendeleo kujikita katika mantiki ya: ubinafsi na faida kubwa mambo ambayo yanasababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira, nyumba ya wote. Maisha ya binadamu yanapaswa kulindwa na kuendelezwa dhidi ya utamaduni wa kifo.

Sera na mikakati ya mipango miji, itoe kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kutambua kwamba binadamu anahitaji familia! Mikakati ya kiufundi inahitaji kuungwa mkono na elimu makini itakayosaidia kuleta mabadiliko katika mtindo wa maisha ya watu ili kuthamini maisha katika makazi ya watu, ili kumwendeleza mtu mzima: kiroho na kimwili! Mwishoni anasema Askofu mkuu Bernardito Auza kwamba elimu na ushirikishwaji wa watu ni muhimu ili kuweza kufikia malengo yanayobainishwa na Jumuiya Kimataifa, ili kila mtu aweze kupata maisha bora kwa kudumisha utu na heshima ya binadamu!

Wakati huo huo kwenye Mkutano wa makazi ya Watu ulioandaliwa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, Askofu mkuu Auza amekazia umuhimu wa kuwa na makazi bora kwa wote, ili kulinda utu na heshima ya binadamu wote. Lengo ni kuhakikisha kwamba, sera na mikakati ya maendeleo endelevu inatoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi. Jumuiya ya Kimataifa iwajibike kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, ili watu waweze kupata fursa za ajira na kuishi kwa amani na utulivu. Watu wanaoishi katika makazi duni wanaathirika sana kwani utu na heshima yao kama binadamu vinawekwa rehani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.