2016-10-30 13:35:00

Jengeni misingi ya haki, amani na utulivu wakati wa kura ya maoni!


Viongozi wa kidini nchini Pwani ya Pembe wanawataka wananchi wote kujenga msingi wa haki, amani na utulivu wakati wa mchakato wa kupiga kura ya maoni, Jumapili tarehe 30 Oktoba 2016. Hili liwe ni zoezi linalojikita katika haki ya wananchi Kikatiba ili kuweza kuchangia mustakabali wan chi yao kwa siku za usoni. Hii ni changamoto ambayo inatolewa na Askofu mkuu Jean- Pierre Kutwa wa Jimbo kuu la Abijan, Pwani ya Pembe.

Ni matumaini yake kwamba, waanchi wameweza kusoma muswada wa katiba mpya inayopendekezwa na hatimaye kufanya maamuzi ya kuukubali au kuukataa wakati wa kupiga kura ya maoni. Askofu mkuu Kutwa anawakumbusha wadau mbali mbali katika siasa kwamba, wananchi wengi wanawaangalia kwa jicho la kengeza na wasi wasi mkubwa kutokana na baadhi yao kuendekeza siasa za ubaguzi na utengano nchini humo, mambo ambayo hayana mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wengi.

Muswada wa Katiba mpya inayopendekezwa ulipitishwa na Bunge kunako tarehe 11 Oktoba 2016. Ili iweze kukubaliwa kuwa ni Katiba mpya, wananchi wanapaswa kuonesha utashi wao kwa njia ya kura ya maoni. Vyama vya upinzani vinavyoungwa mkono na Rais wa zamani Laurent Gbgabo vinawataka wananchi kususia kura hii ya maoni kwa kutojitokeza kwenda kupiga kura.

Iliwachukua wabunge muda mfupi tu kuweza kupitisha vipengele 184 vinavyobainishwa kwenye Katiba mpya, iliyofanyiwa kazi na kamati ya wanasheria na wala si Kamati ya Bunge. Pamoja na mambo mengine, Katiba mpya inayopendekezwa inaunda Baraza la Senate ambalo theluthi ya wajumbe wake watateuliwa na Rais wanchi, Ofisi ya Makamu wa Rais inaundwa pia pamoja na kuondoa vipingamizi kwa watu waliokuwa wanawania nafasi ya Urais nchini humo kwa kuzingatia uraia. Elimu bora na usawa katika elimu sasa ni haki msingi kwa wananchi wote wa Pwani wa Pembe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.