2016-10-29 08:29:00

Safari kuelekea mchakato wa upatanisho!


Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Sweden kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani kuanzia tarehe 31Oktoba hadi tarehe 1 Novemba 2016 ni tukio la kihistoria linaloweka jiwe la msingi katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, umoja na upatanisho kati ya Wakristo! Haya ni matunda ya majadiliano ya kiekumene yaliyofanywa na Kanisa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, baada ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kutoa dira na mwongozo kwa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo!

Hivi ndivyo anavyosema, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV., wakati huu, Baba Mtakatifu Francisko anapoyaelekeza mawazo yake kwenye maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani. Baba Mtakatifu Francisko akiwa mjini Lund na Malmo atashiriki maadhimisho haya ambayo kunako mwaka 1517 Martin Luther aliwasha kibiriti cha mageuzi ya maisha ya kiroho, moto ambao ulienea hata katika masuala ya kisiasa, kijamii na kitamaduni. Matokeo yake Kanisa likatengana na huo ukawa ni mwanzo pia wa vita ya kidini, uchu wa madaraka na mipasuko ya kijamii.

Maadhimisho ya tukio hili kwa miaka mingi yamekuwa ni chanzo cha kinzani na migogoro ya kidini, lakini mwaka 2016, tukio hili linachukua sura na mwelekeo mpya kwa uwepo na ushiriki mkamilifu wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya, chachu ya kuendeleza: toba, wongofu wa ndani, umoja na upatanisho miongoni mwa Wakristo, changamoto kubwa iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Haya ni majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kuvuka vikwazo na kinzani zilizosababisha mpasuko wa Kanisa.

Kardinali Parolin anakaza kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II alishuhudia Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani pamoja na Kanisa Katoliki, yakitiliana sahihi Tamko la pamoja kuhusu “Kuhesabiwa haki ndani ya Kanisa”. Hii ni mada tete iliyokuwa kiini cha malumbano na misigano ya kitaalimungu. Kanisa linaendelea kumshukuru Mungu kwa hatua hii iliyofikiwa na kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani ni fursa nyingine tena ya kihistoria kuweza kuimarisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene na umoja wa Kanisa la Kristo!

Kardinali Parolin anasema kwamba, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuwasili nchini Sweden Jumatatu, tarehe 31 Novemba 2016 na kupokelewa na viongozi wa Serikali na Kanisa, ataitembelea familiya ya kifalme na baadaye Alasiri atashiriki pamoja na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani sala kwa ajili ya maadhimisho haya. Jioni, Baba Mtakatifu Francisko atashiriki tukio la pili ambalo linajikita katika ushuhuda wa kiekumene unaotolewa na Makanisa haya mawili sehemu mbali mbali za dunia.

Hili ni tukio la sherehe na furaha hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya na hapo Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis pamoja na Shirikisho la Huduma la Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani watatiliana sahihi makubaliano ya pamoja katika Uekumene wa huduma, kielelezo cha ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, hususan kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Vijana wa kizazi kipya ndio wadau wakuu wanaohamasishwa na Makanisa haya mawili, kuwa mstari wa mbele kama vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, cheche za matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Kardinali Parolin anakaza kusema, ushuhuda huu utajikita kwa namna ya pekee katika ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na mshikamano unaoongozwa na kanuni auni. Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaoendelea kuhamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana; kwa kushikamana katika matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Huu ni mwaliko wa kuvuka ubinafsi, utepetevu wa imani pamoja na kumezwa mno na malimwengu; mambo ambayo yanaendelea kusababisha kinzani na mipasuko sehemu mbali mbali za dunia. Kumbe, ushuhuda wa pamoja anasema Kardinali Pietro Parolin unalenga kuvunjilia mbali mambo yanayokinzana na tunu msingi za maisha na utume wa Kanisa, ili kushuhudia na kutangaza furaha inayobubujika kutoka katika imani kwa Kristo na Kanisa lake.

Jumuiya ya waamini wa Kanisa Katoliki nchini Sweden ni ndogo, ikilinganishwa na waamini wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri. Jumanne, tarehe 1 Novemba 2016, Baba Mtakatifu Francisko ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Wakatoliki huko Sweden. Ibada hii itaadhimishwa kwenye Uwanja wa Michezo wa Malmo n ahapo atakuwa anakunja vilago vya hija yake ya kitume nchini Sweden kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani.

Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Jumuiya ya Wakatoliki ni chachu ya kuendelea kusonga mbele katika majadiliano ya kiekumene yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini. Wakristo wanapaswa kuonesha mshikamano wa dhati na wakimbizi pamoja na  wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha nchini Sweden. Majadiliano yapewe kipaumbele cha kwanza; kinzani na migogoro ipewe kisogo kwani haina nafasi tena katika maisha na utume wa Kanisa la Kristo! Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anahitimisha mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni cha Vatican kwa kusema kwamba, mchakato wa upatanisho ni nguvu inayowaweka Wakristo huru kwa kuwakirimia matumaini na kuamianiana, huku wakishikamana katika Uekumene wa huduma ya upendo na mshikamano, tayari kuambata huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.