2016-10-29 10:21:00

Papa Francisko: Kashfa ya utengano!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Padre Ulf Jonsson wa Jarida la “Signum” linalomilikiwa na kuchapishwa na Wajesuit huko nchini Sweden wakati huu wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani anasema, majadiliano ya kiekumene ni mchakato unaofanywa kwa Wakristo kukaa kwa upendo na mshikamano kama ndugu pamoja na kutembea katika umoja.

Baba Mtakatifu anasema, katika maisha na utume wake kama Padre, Askofu na sasa Khalifa wa Mtakatifu Petro amebahatika kuwa na marafiki wengi kutoka katika Kanisa la Kiinjili la Kiluteri. Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi tarehe 1 Novemba 2016 anashiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani huko Sweden. Hii ni hija inayojikita kwa namna ya pekee katika ushuhuda wa Uekumene wa huduma na upendo; umoja na mshikamano katika maisha ya kawaida miongoni mwa Wakristo. Baba Mtakatifu anasema, ameamua kuongeza siku moja ya hija yake ya kitume nchini Sweden, ili kutoa nafasi kwa Jumuiya ya Wakatoliki kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu. Anasema, amebahatika kuwa na marafiki wengi waamini wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri, ambao wamemsaidia sana katika hija ya maisha yake ya kiroho na kitume kwa nyakati mbali mbali.

Baadhi yao ni akina Anders Ruuth na Albert Anderson, ambao walijadiliana hata wakati mwingine kwa ukali, lakini katika ukweli na uaminifu kama marafiki. Pale misigano hii ilipokuwa inahatarisha mshikamano wa udugu na upendo, Baba Mtakatifu anasema, alikuwa anachukua uamuzi mapema wa kukutana na rafiki zake, ili kuombana msamaha, tayari kusonga mbele katika majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika uhalisia wa maisha!

Baba Mtakatifu anasema, mageuzi ni sehemu ya mchakato wa maisha ya Kanisa ambayo kwa namna ya pekee kabisa yalisababishwa na Martin Luther. Kimsingi ni kiongozi ambaye aliwarudishia Wakristo Biblia Takatifu, ili iweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao kila siku. Hiki ni kitendo cha kishujaa ambacho Martin Luther alithubutu kukifanya pamoja na kusaidia kurekebisha mapungufu ya kibinadamu yaliyokuwa yanaendelea kulichafua Kanisa la Kristo kwa wakati ule.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wanataalimungu wanayo dhamana na wajibu wao katika kutafakari, kupembua na hatimaye kufikia muafaka kwenye Mafundisho tanzu ya Kanisa. Lakini, ni wajibu wa Wakristo kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika: Sala na huduma ya upendo inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni wajibu wa Wakristo kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Uekumene wa damu inayomiminika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Huu ni Uekumene unaojikita katika Umoja unaopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo, kumbe, hakuna haja ya kuwa na wongofu wa shurutu ndani ya Makanisa haya, kufanya hivi ni kukosa dira na mwelekeo sahihi wa Kiekumene. Kuna Wakristo wanaoendelea kuteswa, kunyanyaswa na kuuwawa kikatili hasa huko Mashariki ya Kati, Ukanda ambao kwa sasa umegeuka kuwa ni Ukanda wa Mashuhuda wa Imani.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, hakuna dini inayoanzisha vita na kwamba, kile kinachodaiwa kuwa ni vita vya kidini ni matokeo ya uchu wa mali na madaraka; chuki na hasira pamoja na watu kupenda kumezwa mno na malimwengu. Dini kimsingi ni mahali pa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu; ustawi na maendeleo ya wengi, haki, amani, upendo na msamaha.

Kanisa halina budi kujiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu ili aweze kulipyaisha kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, ili kuondokana na ukale unaolifanya Kanisa kushindwa kuwa shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake na matokeo yake ni ukanimungu na kutopea kwa imani. Baba Mtakatifu anahitimisha mahojiano yake kwa kusema, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, alimwangalia kwa jicho la huruma, akampenda na kumchagua “Miserando atque eligendo”.

Daraja Takatifu ni zawadi maalum kabisa ambayo ameipokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya huduma kwa Kanisa na Familia ya Mungu katika ujumla wake. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, hija yake ya kitume nchini Sweden itamwezesha kuwaunganisha Wakristo na hivyo kuwa karibu zaidi, ili kweli mchakato wa majadiliano ya kiekumene uweze kusimikwa katika hija ya safari ya pamoja badala ya kuendelea kujifungia katika ubinafsi kwani kwa kufanya hivi, hakuna mageuzi ya kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.