2016-10-29 16:16:00

Maendeleo ya kiuchumi yazingatie usalama wa chakula na lishe bora!


Chakula na lishe bora ni mambo msingi na ya nyakati zote hasa hizi za sasa, katika kutokomeza tatizo la njaa na utapia mlo. Akitoa hotuba yake, Askofu Mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, ameukumbusha mkutano huo kwamba: Ingawa juhudi zimewekwa na Jumuiya ya Kimataifa tangu mwaka 1990 kutokomeza baa la njaa na utapia mlo, bado leo zaidi ya watu milioni 800 hawapati mlo wa kutosha, na zaidi ya watoto milioni 200 wanadumaa au hata kufariki dunia kwa kukosa chakula bora.

Changamoto za kuboresha uzalishaji wa mazao na kukabili mabadiliko ya tabia nchi, zimeongezeka uzito kutokana na mahangaiko ya uhamaji wa watu ndani na nje ya nchi, vita, machafuko, mambo ambayo yamekimbiza wengi kutoka maeneo ya uzalishaji. Ni Dhahiri kwamba, bila siasa tulivu na uwajibikaji wa jamii nzima, malengo ya maendeleo na afya bora kufikia 2030 itakuwa ngumu kuyafikia.

Baba Mtakatifu Francisko anaonya dunia kuwa makini, kutotazama tatizo la njaa na umaskini wa kupindukia, kana kwamba ni jambo asili au la kawaida na kuishia kutafuta hesabu za wahanga, badala yake anaalika kila mmoja kujisikia ulazima wa kuwajibika kuhakikisha jibu la kudumu linatafutwa. Baba Mtakatifu Francisko anakazia kusema, mali zilizopo duniani zinatosha kwa wote iwapo zitatumika kwa Ukarimu na kujali wengine, cha ajabu leo hii, badala ya kutumika kulisha watu zinatumika kulisha vita, ndiyo sababu baadhi ya sehemu watu wanakula na kusaza, wakati sehemu zingine watu wanfariki kwa njaa. Kutokana na ukweli huo, Askofu Mkuu Auza ansema, ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030 ya kutokomeza njaa, ni lazima kuhakikisha Amani, haki, mshikamano, huruma na kujali wengine vinazingatiwa ili kuwatambua wenye njaa na kiu wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia!

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.