2016-10-28 07:34:00

Ukweli na uwongo; wema na ubaya ni mambo yanayosigana!


Kardinali Gerhard Ludovic Muller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa ameandika kitabu kuhusu Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI na Papa Francisko katika ulimwengu wa utepetevu wa imani na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Kardinali Muller anapembua kwa kina na mapana mipaka katika ukweli na uwongo; kati ya wema na ubaya; mambo ambayo daima yanasigana na kukinzana!

Hii ni changamoto kubwa kwa viongozi wa Kanisa, waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete ili kupambana na magonjwa haya ya maisha ya kiroho yanayoendelea kuwatesa watu wengi duniani! Baba Mtakatifu Benedikto XVI na Papa Francisko ni viongozi wanaojikita katika masuala ya kitaalimungu na kichungaji, kila mtu akijitahidi kuchangia kadiri ya uwezo wake pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati.

Kardinali Muller anasema katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 10 tangu Baba Mtakatifu Benedikto XVI alipochaguliwa kuliongoza Kanisa, hapo tarehe 17 Aprili 2015, baada ya kuhariri kitabu cha kazi za kitaalimungu za Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, aliamua kuandika tena kitabu ambacho ni tafakari na upembuzi wa kina na mapana juu ya changamoto mamboleo ambazo Kanisa linakumbana nazo katika ulimwengu mamboleo. Anajadili dhamana na wajibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika ulimwengu mamboleo.

Kardinali Muller anaangalia dhamana na mchango wa waamini walei; Umoja wa Kanisa na mchakato wa majadiliano ya kiekumene; Ushiriki mkamilifu wa utume wa Kanisa na utakatifu wa maisha ya Kikristo kama kielelezo makini na chenye mvuto na mashiko katika dhamana ya Uinjilishaji mpya! Changamoto zote hizi zimevaliwa njuga na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI pamoja na Papa Francisko, kila kiongozi akijitahidi kwa moyo, akili na karama zake kujibu changamoto hizi pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati.

Haya ndiyo mambo makuu ambayo Kardinali Muller anapenda kuwashirikisha wasomaji wake katika kitabu hiki kipya. Anagusia kwa namna ya pekee, changamoto ya utu na heshima ya binadamu katika ulimwengu mamboleo kutokana na misimamo mikali ya kiimani, vita na kinzani za kitaifa na kimataifa. Mambo yote haya yanaligusa pia Kanisa la Kristo linaloongozwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwani Kanisa linaishi na kutenda shughuli na utume wake wa Kisakramenti katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu kutokana na karama na dhamana aliyokabidhiwa ya kuliongoza Kanisa la Kristo anayo nafasi kubwa ya kuwasaidia walimwengu kuwa na matumaini mapya, kwa kutambua kwamba, hapa duniani wao ni wasafiri na wala hawana makao ya kudumu, bali wanapaswa kujiwekea hazina yao kwenye Yerusalemu ya mbinguni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.