2016-10-28 08:51:00

Kilio cha wananchi wa Sudan ya Kusini!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 27 Oktoba 2016 amekutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Makanisa nchini Sudan ya Kusini. Askofu mkuu Paulino Lukudu Loro wa Jimbo kuu la Juba; Askofu mkuu Daniel Deng Bul Yak wa Kanisa la Kiaskofu Sudan pamoja na Mheshimiwa Peter Gai Lual Marro, Mratibu wa Kanisa la Kipresibiteriani. Katika mazungumzo yao, Baba Mtakatifu pamoja na viongozi hawa wa Makanisa wamegusia kwa uchungu mkubwa vita inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao; kwa umoja na mafungamano ya kijamii nchini Sudan ya Kusini.

Viongozi hawa wameangalia umuhimu wa kukuza na kudumisha misingi ya amani na utulivu pamoja na kuendeleza ushirikiano kati ya Makanisa nchini Sudan ya Kusini kwa ajili ya ustawi, maendeleo, utu na heshima ya binadamu pamoja na mafao ya wengi. Ni wajibu wa Makanisa kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea wanyonge na maskini ndani ya jamii sanjari na kuendeleza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili hatimaye upatanisho na umoja wa kitaifa viweze kushika tena mkondo wake.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Kanisa Katoliki, yamekuwa ni muda muafaka wa toba, wongofu wa ndani; uzoefu na mang’amuzi ya msamaha na ukarimu kama njia ya kujenga, kukuza na kudumisha misingi ya amani na maendeleo endelevu ya binadamu yanayogusa mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili. Makanisa nchini Sudan ya Kusini yakiwa yamejikita katika umoja na mshikamano, kwa ajili ya huduma ya familia ya Mungu nchini humo, yameendelea kuwa mstari wa mbele kusaidia mchakato wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na kusaidiana.

Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wa Makanisa kutoka Sudan ya Kusini kwa mara nyingine tena, wameonesha umuhimu wa kufanya hija ya pamoja na kuendelea kushirikiana katika misingi ya kuaminiana na matumaini mapya,  ili kuwawezesha wananchi wa Sudan ya Kusini kuwa na uhakika wa usalama wa maisha yao na leo pamoja na kesho iliyo bora zaidi. Mchakato huu unaweza kuimarishwa kwa Makanisa haya kutumia Mapokeo na utajiri wake wa maisha ya kiroho kwa ajili ya mafao ya wengi!

Wakati huo huo, viongozi wa Makanisa wakati wakizungumza na waandishi wa habari mjini Vatican wanasema, wako mjini Roma, ili kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kusaidia juhudi za kumaliza vita na mipasuko ya kijamii nchini Sudan ya Kusini. Vita hii inaendelea kuchowewa na misingi ya ukabila na udini usiokuwa na mashiko wala mvuto kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wa Sudan ya Kusini. Watu wanaendelea kuteseka kutokana na magonjwa, njaa na ujinga kwani watoto wanashindwa kwenda shuleni kutokana na vita, kinzani na migogoro iliyopo. Viongozi wa Makanisa Kusini mwa Sudan wanasema, wamemwelezea Baba Mtakatifu Francisko hali halisi, ili hatimaye, Jumuiya ya Kimataifa iweze kutambua jinsi wananchi wa Sudan ya Kusini wanavyoteseka. Hata kama inawezekana, Jumuiya ya Kimataifa itume kikosi cha askari wa kulinda amani. Ni matumaini ya familia ya Mungu nchini Sudan kwamba, iko siku wataweza kumwona Baba Mtakatifu Francisko, mjumbe wa amani, matumaini na huruma ya Mungu akiwa kati yao, ili kuwafariji na kuwatia shime kusonga mbele. Itapendeza zaidi, ikiwa kama Papa Francisko atakua ameandama pia na Askofu mkuu Justin Welby, Mkuu wa Kanisa Anglikani, kielelezo cha mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika huduma ya upendo na mshikamano.

Sudan ya Kusini, ilijipatia uhuru wake wanasema viongozi wa Makanisa, lakini kwa bahati mbaya hawakuweza kuwajibika vyema katika kuulinda na kuudumisha kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi na matokeo yake baadhi ya watu wanataka kujinufaisha wakati maelfu ya watu wakiteseka kwa vita, njaa, maradhi na ujinga. Ukabila na udini; uchu wa mali na madaraka ni mambo yanayoitesa Sudan ya Kusini kwa sasa.

Viongozi wa Makanisa wanasema, wamekutana na Baba Mtakatifu Francisko, katika umoja wao, ili kuomba amani kwa ajili ya wananchi wa Sudan ya Kusini sanjari na kuendeleza mchakato wa haki, amani na upatanisho. Baba Mtakatifu amewahakikishia uwepo wake kwa njia ya sala na sadaka yake. Viongozi wa Makanisa Sudan ya Kusini wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko ambaye anaendelea kujitambulisha kuwa ni mtu wa watu, mjumbe na chombo cha haki, amani na maridhiano kati ya watu na kwamba, anasikitika kutoka na hali tete inayoendelea huko Sudan ya Kusini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.