2016-10-28 15:53:00

Biashara ya binadamu na utumwa mamboleo unapokonya utu wa binadamu


Kikundi cha Mtakatifu Martha ni taasisi ya kimataifa dhidi ya biashara haramu ya binadamu kilichozinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2014 ili kupambana na donda hili la kijamii linalodhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa kuwatumbukiza watoto, wasichana na wanawake katika utumwa mamboleo. Kikundi cha Mtakatifu Martha, baada ya mkutano wake wa siku mbili, kimepata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 27 Oktoba 2016 ili kuwasilisha sera na mikakati ambayo imefanyiwa kazi katika kipindi cha miaka miwili.

Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles anasema, kumekuwepo na mwamko mkubwa na uelewa wa madhara ya biashara ya binadamu na utumwa mamboleo katika maisha ya watu, hasa zaidi maskini. Kikundi hiki kimeanza kutoa huduma kwa waathirika wa vitendo hivi vya kinyama vinavyoficha ukatili dhidi ya ubinadamu. Kuna watu wanaoteseka, lakini kwa bahati mbaya kilio chao hakiwezi kusikika ni sawa na machozi ya samaki, yameishia baharini.

Kikundi cha Mtakatifu Martha, kimewaonesha walimwengu madhara ya biashara haramu ya binadamu pamoja na kusikiliza shuhuda mbali mbali zilizotolewa na baadhi ya wahusika wakati Kikundi hiki kilipokuwa kinazungumza na waandishi wa habari. Bi Princess Inyang kutoka Nigeria anasema, kunako mwaka 1999 alisafirishwa na wafanyabiashara ya binadamu kwenda Ulaya, kwa matumaini ya kupata fursa ya ajira nzuri na kwamba, huo ungekuwa ni mwanzo wa mchakato wa kuupatia umaskini kisogo. Lakini alipofika Italia, akajikuta anatumbukizwa kwenye biashara ya ngono barabarani na kile kidogo alichokuwa anakusanya kutoka kwa wateja wake, ilimbidi kukiwasilisha kwa Boss aliyekuwa amemnyang’anya hati zote za kusafiria.

Bi Inyang baada ya mateso makali na machungu ya kudhalilishwa utu wake, siku moja akabahatika kukutana na wasamaria wema, waliomwezesha kuchomoka kwenye mtego na leo hii yuko huru na kwamba, ameanzisha kikundi kinachowasaidia wasichana na wanawake kujinasua kutoka kwenye mitego ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ndani na nje ya Nigeria. Ameanzisha kituo cha kupima na kutoa ushauri nasaha kwa waathirika wa Ukimwi. Amefanikiwa kuwashawishi wasichana wengi huko Edo kutokubali kutumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Lakini, wafanyabiashara hawa bado wanaushawishi mkubwa kwa vijana wanaotaka maisha ya kubweteka kwa kudhani kwamba, Ulaya “mambo yote ni sawa na maji kwa glasi” na kusahau kuwa, kuna watu wanaoteseka kwa ukosefu wa fursa za ajira, umaskini na upweke! Jumuiya ya Kimataifa inaweza kupambana na biashara hii haramu kwa kuhakikisha kwamba, sheria za kitaifa na kimataifa zinatekelezwa kwa dhati kwa kuzingatia nidhamu na uadilifu wa kazi. Maboresho ya sekta ya elimu yanaweza kusaidia kupambana na vishawishi vya kudhani kwamba, mambo mazuri yanapatikana Ulaya peke yake, kumbe, vijana wajengewe ari na moyo wa uzalendo wa kupenda nchi yao. Vyombo vya usalama kimataifa viwatafute na kuwashughulikia wadau wote wa biashara haramu ya binadamu ili kuvunjilia mbali mnyororo huu unaowapora watu utu na heshima yao kama binadamu. Waathirika wasaidiwe ili kuanza kuandika tena ukurasa mpya wa maisha yao kwa maisha mazuri zaidi.

Al Bangura kutoka Sierra Leone anasema, alijikuta anatumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu baada ya wazazi wake kufariki dunia wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone. Akashawishiwa kutafuta maisha bora zaidi nje ya Sierra Leone. Akabahatika kufika Guinea na huko akakutana na watu waliohakikishia kwamba, angeweza kupata nafasi ya kuchezea Timu kubwa Barani Ulaya kwa vile alikuwa na kipaji cha kutandaza kabumbu kama Pelle. Akasafirishwa hadi Uingereza, akarudishwa na kutelekezwa nchini Ufaransa na baadaye kurejeshwa tena nchini Uingereza.

Mwishoni, alibahatika kupata kocha aliyemsaidia kumwingiza na hatimaye, kuchezea timu moja huko Uingereza. Lakini mateso na mahangaiko aliyopata yamemshikisha adabu katika maisha na kwamba, hasingependa kuwaona vijana wenzake wakiteseka kama alivyoteseka kwa vile tu walikuwa na ndoto ya kwenda Ulaya kula kuku kwa mrija!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.