2016-10-27 08:07:00

Ujasiri wa Papa Francisko: Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani


Dr. Martin Junge, Katibu mkuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano anasema, ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani ni uamuzi wenye ujasiri na imani kubwa. Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi tarehe 1 Novemba 2016 kufanya hija ya kitume huko Lund, nchini Sweden

Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani ni kumbu kumbu endelevu iliyotoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Mkombozi wa ulimwengu; Umuhimu wa ufahamu wa Neno la Mungu linalotafsiriwa na kueleweka na waamini katika lugha zao, ili liweze kuwa ni taa na mwanga katika mapito ya Wakristo hapa duniani na kwamba, imani inapaswa kufahamika kuwa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kumwilishwa katika matendo, kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji!.

Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri kwa pamoja yanaadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipoanzisha mchakato wa majadiliano ya kiekumemene, tukio ambalo litafikia kilele chake hapo mwaka 2017. Makanisa haya yanapenda kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Makanisa yanataka kutoa kipaumbele cha pekee kwa mambo msingi yanayowaunganisha Wakristo badala ya kuendekeza yale ambayo yamesababisha kinzani na utengano katika historia, utume na maisha ya Kanisa la Kristo! Yesu mwenyewe katika ile sala yake ya kikuhani anaombea umoja wa wafuasi wake, changamoto ambayo inaendelea kufanyiwa kazi katika majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika Uekumene wa sala, huduma na ushuhuda wa pamoja.

Hiki ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, kwa kutambua na kuguswa na mahangaiko ya watu mbali kutokana na vita vya kidini, chuki na uhasama vilivyosababishwa na Mageuzi ya Kiluteri Duniani. Malumbano ya kitaalimungu yalivamiwa na wanasiasa na wachumi na matokeo yake yakawa ni vita vya kidini na mipasuko ya kijamii, mambo ambayo pengine hata leo hii bado yanaonesha ukakasi katika maisha ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia!

Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, mahusiano ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri nchini Sweden yameboreka kwa kiasi kikubwa. Kuna majadiliano ya kiekumene yanayofanyika katika ngazi mbali mbali ya maisha na utume wa Kanisa nchini humo. Ni majadiliano yanayojikita katika ushuhuda wa Uekumene wa huduma, upendo na ukarimu hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Dr. Martin Junge anakaza kusema, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walianzisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI na Papa Francisko wanaendelea kusukuma mbele mchakato huu kwa ajili ya umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa waamini. Ni viongozi ambao wanaendelea kuhamasisha umuhimu wa kutafuta na hatimaye, kujikita katika ukweli na uwazi kama nyenzo msingi, kuelekea umoja wa Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1999 aliwasaidia wanataalimungu kufikia makubaliano ya kimsingi na hatimaye, Makanisa haya mawili yakatoa tamko la pamoja kuhusu “ Mafundisho ya kuhesabiwa haki ndani ya Kanisa”.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2013 akaridhia Waraka kuhusu “Kutoka katika kinzani, kuelekea katika Umoja”. Kwa sasa Baba Mtakatifu Francisko amefanya uamuzi wa kijasiri, kwenda kushiriki moja kwa moja katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani huko Lund, Sweden. Hii ni sehemu ya mchakato wa uimarishaji wa majadiliano ya kiekumene yaliyoanzishwa na Makanisa haya mawili, miaka 50 iliyopita, kiasi kwamba, waamini wa Makanisa haya wanajisikia kuwa karibu zaidi, ikilinganishwa na miaka 50 iliyopita, wakati Makanisa yalikuwa yanawaka moto wa chuki na hasira!

Kwa muda wa miaka kadhaa, viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki wametembelea Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri sehemu mbali mbali za dunia. Lakini kwa mwaka huu, Baba Mtakatifu Francisko ataungana na Askofu Munib Younan pamoja na viongozi wakuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilei hii ambayo kwa miaka mingi ilikuwa ni sababu ya kinzani na mipasuko ndani ya Makanisa!

Uwepo wa Baba Mtakatifu katika maadhimisho haya ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaojikita katika Uekumene wa sala, huduma, upendo na mshikamano kwa kukazia zaidi tunu msingi za maisha ya Kikristo zinazowaunganisha badala ya kuendekeza yale mambo yanayowagawa na kuwavuruga Wakristo! Makanisa haya yanapenda kuangalia historia iliyopita kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani; kuchuchumilia ya mbeleni kwa moyo wa shukrani na ujasiri; changamoto ambayo iko mbele ya Wakristo wakati huu wa mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, ili kwa pamoja waweze kushikamana na hatimaye, kukabiliana na mawimbi ya ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia!

Maadhimisho haya ni chachu ya umoja, upendo na upatanisho kati ya Makanisa haya mawili, ili kuondokana na shutuma zilizosababishwa na malumbano, kinzani na mitafaruku ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Upatanisho utakaowawezesha waamini wa Makanisa haya mawili kuadhimisha kwa pamoja Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Katika matukio yote haya Kristo Yesu, chemchemi ya upatanisho na ufunuo wa huruma ya Baba wa mbinguni, asaidie kudumisha nia hii njema, ili wote kwa pamoja waweze kupokea zawadi na huruma ya Mungu katika maadhimisho mbali mbali. Umoja wa imani, ushuhuda wa huduma ya huruma, upendo na mashikamano kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni mambo msingi sana katika mchakato wa mwendelezo wa majadiliano ya kiekumene wakati huu wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani.

Martin Luther alitoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu kuwa ni Mkombozi wa Ulimwenguni, akataka Bibilia iweze kufahamika na watu wengi, ili Neno la Mungu liwe ni taa, dira na mwongozo wa maisha. Wakristo wote wanapata chimbuko na utambulisho wao katika Sakramenti ya Ubatizo. Umefika wakati kwa Wakristo kusimama kidete, kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma, upendo na mshikamano unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.