2016-10-27 15:07:00

Lindeni na kudumisha Injili ya ndoa na familia!


Taasisi ya Yohane Paulo II imeundwa kwa wakati muafaka kutokana na busara, hekima na mang’amuzi ya shughuli za kichungaji yaliyoasisiwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, kwa kusoma alama za nyakati, ili kuendeleza agano la upendo kati ya bwana na bibi katika maisha ya ndoa na familia. Taasisi hii imekua na kupanuka sehemu mbali mbali za dunia kiasi kwamba, imepata chapa ya Ukatoliki katika sera, mikakati na mipango yake. Taasisi hii ni kitovu cha majadiliano ya kina na taasisi mbali mbali zinazojikita katika masuala ya kidini na kitamaduni zinazojadili masuala tete yanayomsibu binadamu katika ulimwengu mamboleo!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 27 Oktoba 2016 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Taasisi ya Yohane Paulo II inayojihusisha kikamilifu na masuala ya ndoa na familia. Mahusiano na mafungamano ya watu wa ndoa yanakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na ubinafsi, kutopea kwa imani pamoja na watu wengi kupenda kumezwa na malimwengu. Matokeo yake ni watu kuwa na mawazo ya uhuru tenge, kutowajibika barabara pamoja na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, sera tenge dhidi ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na umaskini ni mambo yanayohatarisha mustakabali wa familia kwa siku za usoni, bila kusahau teknolojia mamboleo inayokinzana na utu, heshima na maisha ya binadamu. Kutokana na changamoto hizi, kuna haja ya kuwa na uhusiano wa karibu kati ya Taasisi ya Yohane Paulo II na Taasisi ya Kipapa ya Maisha, ili kuwa na mwelekeo mpana zaidi katika kukabiliana na changamoto hizi. Kuna haja ya kuondokana na falsafa ya ubinafsi na kuanza kujielekeza zaidi kwenye mang’amuzi ya agano kati ya bwana na bibi.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, agano hili linajikita kwa namna ya pekee katika ushirikiano na kuheshimiana; sadaka na majitoleo; uwajibikaji shirikishi; kwa kutambua na kuheshimu tofauti zilizopo kati ya bwana na bibi kama utajiri mkubwa unaopaswa kulindwa na kudumishwa. Kuna haja pia ya kuthamini utu na heshima ya binadamu pamoja na mahusiano yao. Ni vigumu kuweza kufumbia macho utamaduni mamboleo unaotambua thamani ya utofauti wa kijinsia; lakini kwa bahati mbaya utamaduni huu unataka kufutilia mbali tofauti za kijinsia!

Tumbo la mama mzazi ni mahali pa kwanza kabisa ambapo agano kati ya waanadamu linafanyika, kadiri ya neema ya Mungu na hatimaye, kusambaa katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Mahusiano yanayofumbatwa katika agano hili yanakuza na kudumisha mahusiano ya kidini, kimaadili, kikazi, kiuchumi, kisiasa na kati ya vijana wa kizazi kipya na vijana wa zamani. Pale ambapo mahusiano na mafungamano haya ya kijamii yanakwenda salama, dunia inaendelea kusonga mbele, kinyume chake, dunia inageuka kuwa chungu na historia ya binadamu inadumaa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ushuhuda wa ubinadamu na uzuri wa uzoefu na mang’amuzi ya Kikristo kuhusu familia yasaidie kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Kanisa lina wajibu wa kugawa upendo wa Mungu kwa ajili ya utume wa familia sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa linajitambua kuwa ni familia ya Mungu, Fumbo kubwa linalofanya rejea kwa Kristo na Kanisa lake; dhamana inayotekelezwa kwa njia ya upendo na mikakati ya shughuli za kichungaji ili kukuza na kuendeleza: ukweli na uzuri wa mpango wa Mungu katika kazi ya Uumbaji; dhamana inayohitaji akili ya upendo na majitoleo ya Kiinjili; upendo na huruma kutokana na udhaifu wa binadamu.

Ili kukabiliana na changamoto hizi, Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna haja kwa Mama Kanisa kujikita kikamilifu katika mafundisho tanzu, mikakati ya shughuli za kichungaji na ushuhuda wenye mvuto na mashiko, ili kukuza mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu sanjari na kueneza upendo wake kwa wote. Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinahifadhiwa katika chombo dhaifu cha mwili wa binadamu ambao unaweza kupata neema, lakini pia unaelemewa na dhambi. Dhana ya ndoa na familia inapaswa kujikita katika uhalisia wa maisha ya watu na wala lisiwe ni jambo la kufikirika. Lengo ni kusaidia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kuwa na mvuto unaojikita katika uaminifu na udumifu.

Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu wote kuungana naye ili kusaidia kuimarisha upendo wa Mungu unaopitia katika maisha ya mwanadamu. Wosia wa kitume “Furaha ya upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” una utajiri mkubwa kwa ajili ya familia ya Mungu ili kutambua mwelekeo wa Kanisa mintarafu maisha ya ndoa na familia. Kuna haja ya kukuza na kudumisha ukweli na uzuri wa maisha ya ndoa na familia kadiri ya Mafundisho ya Kanisa, pamoja na kuwavuta vijana waweze kufunga ndoa na kuendeleza upendo wao kwa Kristo na Kanisa lake, alama wazi ya upendo aminifu na huruma ya Mungu kwa waja wake.

Baba Mtakatifu anaitaka Taasisi ya Yohane Paulo II kulisaidia Kanisa kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara, ili kuganga na kuponya madonda ya: kinzani na utengano katika maisha ya ndoa na familia. Lengo ni kuinjilisha na kuendeleza shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa kwa kujikita katika Ufunuo na Mapokeo ya Kanisa kama njia ya kurithisha imani. Dhamana hii inapaswa kutekelezwa kwa furaha ya imani, unyenyekevu pamoja na huduma inayotolewa na Mama Kanisa, mtumishi asiye kuwa na faida.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.