2016-10-27 15:29:00

Kongamano la kimataifa kuhusu maisha ya kitawa na kazi za kitume!


Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, kuanzia tarehe 28 – 29 Oktoba 2016, linaadhimisha Kongamano la Kimataifa kwa ajili ya wawakilishi wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki pamoja na Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Watawa Duniani, Baba Mtakatifu aliwataka viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba wanaendeleza, wanahamasisha, kuwasaidia watawa kufanya mang’amuzi ya kina na mapana katika karama za mashirika yao; huku wakijitahidi kuwa karibu zaidi kwa huruma na mapendo, kwa Mashirika ya kitawa yanayokabiliwa na hali ngumu ya maisha.

Viongozi wa Kanisa wawe karibu na Mashirika haya kwa kusaidia kuifunda familia ya Mungu kutambua umuhimu wa maisha ya kitawa na kazi za kitume, ili kuwawezesha kusambaza uzuri na utakatifu wa Kanisa. Kwa kuzingatia mwanga na ufahamu huu, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume limeandaa Kongamano la Kimataifa kwa wawakilishi wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki na Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Hawa ni viongozi wanaojihusisha kwa namna ya pekee na masuala ya kuhamasisha na kukuza miito, ili kujenga na kuimarisha umoja wa kikanisa sanjari na umoja wa Kanisa mahalia. Huu ni muda wa kutafakari uhusiano uliopo kati ya viongozi a Kanisa na watawa, hali ambayo wakati mwingine si rahidi sana kutokana na karama na ukweli wa maisha ya kitawa na kazi za kitume. Huu ni muda muafaka wa Baraza hili la Kipapa kubainisha mwongozo pamoja na nyaraka ambazo lina tumaini kuzichapisha kwa siku za usoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.