2016-10-27 16:00:00

Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Waluteri Duniani: Uekumene wa maisha


Baba Mtakatifu Francisko anasema majadiliano ya kiekumene ni mchakato unaofanywa na waamini kwa kutembea pamoja: kwa kusali, kwa kuhudumia na kumtangaza Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Ni mchakato unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini ili kujenga msingi wa majadiliano yatakayowasaidia wanataalimungu kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika mafundisho tanzu ya Kanisa, ili wote kwa pamoja waweze kuwa na umoja.

Baba Mtakatifu wakati wa hija yake ya kitume, kuanzia tarehe 31Oktoba hadi tarehe 1 Novemba, 2016 anasema Dr.  Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican, Baba Mtakatifu pamoja na ujumbe wa Vatican watapanda Bus moja na viongozi wakuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri kutoka mjini Lund hadi Malmo, huko Sweden. Hii itakuwa ni fursa kwa viongozi wa Makanisa haya kupata nafasi ya kubadilishana mawazo katika maisha ya kawaida, changamoto inayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene.

Watakapofika mjini Malmo, viongozi hawa watapanda pia magari ya umeme, kuonesha umuhimu wa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote. Wakristo katika ujumla wao kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira, kwani athari za mabadiliko ya tabianchi ni tishio kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na matokeo yake ni kinzani na mipasuko ya kijamii inayoendelea kutikisa medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu!

Baba Mtakatifu akiwa nchini Uswiss katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani anatarajiwa kutoa hotuba tatu, ambazo atazisoma kwa lugha la Kihispania, ili kumpatia nafasi ya kuweza kuwasilisha vyema ujumbe uliomo kwenye sakafu ya moyo wake, wakati huu Kanisa linapoendelea kujikita katika ushuhuda wa upendo na mshikamano. Hii ni hija ya 17 ya Kimataifa kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko na Sweden inakuwa ni nchi ya 26 kutembelewa na Papa Francisko.

Maadhimisho haya yatawawezesha viongozi wakuu wa Makanisa kusali kwa pamoja; kusikiliza shuhuda za Uekumene wa upendo na huduma unaotekelezwa na waamini wa Makanisa haya mawili kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Tukio hili litafanyika kwenye Uwanja wa michezo wa Malmo, huko Uswiss. Hizi ni juhudi zilizoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis pamoja na Muungano wa Mashirika ya huduma kutoka katika Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.