2016-10-27 16:35:00

Bado Mungu anaendelea kuwalilia watu wake!


Hata leo Mungu analia kuona wanadamu wanateseka na pengine kufa kwa majanga asilia, vita, ibada kwa fedha na mali, na kwa namna ya pekee watoto wanao uwawa. Ni sehemu ya maneno ya Baba Mtakatifu Fransisko katika mahubiri yake, alipokuwa akisali Misa Takatifu kwenye Kikanisa kidogo cha Mt. Martha, mjini Vatikani, siku ya Alhamisi 27 Oktoba 2016. 

Katika Injili,  Yesu anamwita Mfalme Herode Mbweha, yaani mwenye nia mbaya ya kutaka kumuua, na anaonesha utayari wake wa kukikumbatia kifo hicho. Yesu baada ya maneno hayo anaugeukia Mji wa Yerusalemu uliojifunga bila kujitambua, kisha anaanza kuongea kwa upole na huzuni: “Yerusalemu, Yerusalemu, mara ngapi nimewakusanya wanao kama kuku akusanyavyo vifaranga chini ya mbawa zake, lakini hukutaka”.  Kristu anaililia Yerusalemu iliyo na tabia ya kuwaua manabii wanaotumwa katika mji huo. Hii ni sauti ya Baba anayelilia watoto wake wanaopotea. Baba Mtakatifu anatofautisha kilio hiki na kilio cha Yesu mbele ya kaburi la Lazaro. Mbele ya kaburi la Lazaro ni kilio cha rafiki, lakini katika hili la kuuwa watumishi wa Mungu wasio na hatia, ni kilio cha Baba anayelilia watoto waliopotea, ili wapate kurudi.

Kama Baba wa mwana mpotevu, yaani Baba mwenye huruma, baba huyu anasubiri kwa hamu kurudi kwa mwanae, na kila siku anainua macho kwa matumaini ili amuone mwanae akirudi. Kilio hicho cha Baba Mungu, kinanuia kuumba upya kila kiumbe kupitia nafsi ya pili ya Mungu, yaani Bwana wetu Yesu Kristo. Baba Mtakatifu Francis amegusia pia maneno ya Yesu alipokuwa akielekea Calvari, wanawake walipomlilia aliwajibu: “msinililie mimi, walilieni watoto wenu”. Katika kilio hicho cha baba na mama, Mwenyezi Mungu anaendelea leo kulilia wanae. Mungu analia leo kuona watu wengi wanauwawa kwa machafuko, vita, kwa dhuruma, na tamaa ya mali. Ni muhimu kutafakari kilio hicho Mungu anachowalilia wanadamu, na kufanya hima kuzuia mambo yanayopelekea mahangaiko hayo.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.