2016-10-24 15:21:00

Utengenezaji na usambazaji wa silaha za kinyuklia ni kosa la kimaadili!


Viongozi wa Kanisa wamekuwa mstari wa mbele kupinga utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia kutokana na madhara yake makubwa kwa maisha ya binadamu na mali zake. Athari zilizojitokeza baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia huko Hiroshima na Nagasaki ni fundisho kubwa kwa binadamu anayepaswa kujizatiti katika kutafuta na kudumisha misingi ya amani na udugu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko.

Vatican inapenda kuungana na watu wote wenye mapenzi mema wanaoendelea kupaaza sauti zao wakitaka kusitishwa kwa utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia kadiri ya Mkataba wa Kuzuia Utengenezaji wa Silaha za Kinyuklia. Ulimbikizaji wa silaha za kinyuklia ni kielelezo cha taifa kutojiamini katika masuala ya ulinzi na usalama kutokana na kuwa na ndoto ya amani. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Monsinyo Simon Kassas kwa niaba ya Askofu mkuu Bernadito Auza, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa kwenye kikao kilichokuwa kinazungumzia kuhusu udhibiti wa utengenezaji, ulimbikizaji na matumaini ya silaha za kinyuklia.

Umilikaji wa silaha za kinyuklia ni kosa kubwa kimaadili na kwamba, Umoja wa Mataifa hauna budi kuhakikisha kwamba unasimama kidete kwa ajili ya huduma kwa binadamu na mafao ya wengi ili hatimaye kuondokana na kitisho cha uwepo wa silaha za kinyuklia. Amani na utulivu katika medani za kimataifa haiwezi kupatikana kwa kulimbikiza silaha za kinyuklia. Amani ya kweli haina budi kujikita katika msingi ya haki, maendeleo ya kijamii na kiuchumi; uhuru na utunzaji wa utu na heshima ya binadamu; ushiriki wa watu wote katika masuala ya kijamii sanjari na kujenga utamaduni wa watu kuheshimiana na kuthaminiana.

Nchi zinazomiliki, kutengeneza na kusambaza silaha za kinyuklia hazina budi kuondokana na dhana hii kadiri ya maelekezo yaliyotolewa na Jumuiya ya Kimataifa katika kipindi cha miaka 8 iliyopita. Mkutano wa 2017 iwe ni fursa ya kupima mafanikio yaliyokwisha kupatikana hadi sasa. Jumuiya ya Kimataifa katika kipindi cha miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa kupiga marufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi na silaha za nyuklia inaendelea kuyahamasisha mataifa yanayomiliki silaha hizi kuridhia mkataba huo ili uweze kuanza kutumika, ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.