2016-10-24 07:42:00

Madhara ya vita huko Mosul, Iraq ni makubwa kwa watu wote!


Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 23 Oktoba 2016 aliyaelekeza macho na mawazo yake kwa familia ya Mungu nchini Iraq, lakini kwa namna ya pekee kwa wananchi wanaoishi mjini Mosul, ambao wanaendelea kuteseka kutoka na vita ambayo imepamba moto kwa kipindi kirefu na madhara yake yanaonekana kwa wananchi wote wa Iraq wasiokuwa na hatia! Wawe ni waamini wa dini ya Kiislam, Wakristo au waamini wa dini na makabila tofauti tofauti nchini Iraq.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, amepokea kwa uchungu mkubwa taarifa za mauaji ya kinyama waliyotendewa wananchi wa Iraq, wengi wao wakiwa ni watoto wadogo. Ukatili na unyama wa aina hii unawafanya wapenda amani duniani kutoa machozi ya uchungu, huku wakibaki wakiwa wameduwaa! Baba Mtakatifu anataka kuwahakikishia wananchi wote wa Iraq pasi na ubaguzi uwepo wake wa karibu kwa njia ya mshikamano katika sala, ili Iraq ambayo imejaribiwa kwa kiasi kikubwa, iweze kuwa na nguvu na imara katika matumaini, huku ikisonga mbele katika usalama, upatanisho na amani. Baba Mtakatifu Francisko alitumia muda huo kuwaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali katika ukimya, ili kuwaombea wananchi wa Iraq na baadaye, wote kwa pamoja wakasali salam Maria, ili kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria Malkia wa amani!

Baba Mtakatifu mwishoni, aliwasalimia maelfu ya mahujaji na wageni kutoka ndani na nje ya Italia, lakini kwa namna ya pekee kabisa, mahujaji kutoka Poland ambao wamekuwepo mjini Roma kwa ajili ya hija ya maadhimisho ya Miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland. Amewataka waamini wote kusonga mbele kwa imani na matumaini katika hija ya imani, huku wakimkumbuka na kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa njia ya sala!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.