2016-10-24 08:08:00

Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa, 2016


Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 24 Oktoba 2016 inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 71 tangu Umoja wa Mataifa, kipindi ambacho kwa sasa kinakumbana na mabadiliko makubwa kwa Umoja wa Mataifa na ulimwengu katika ukumla wake. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-moon katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku hii anasema, kuna haja kwa Jumuiya Kimataifa kujikita katika dhamana iliyojitwalia ya utekelezaji wa ajenda za Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Kuna Malengo 17 yanayoapswa kutekelezwa ili watu wote waweze kuwa na maisha bora na dunia iwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Jumuiya ya Kimataifa inaanza kuwa na mwelekeo mpya wa maendeleo unaopania kupunguza kiwango cha joto duniani pamoja na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na ongezeko la hewa ya ukaa. Makubaliano ya Itifaki ya Paris kuhusu udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi itaanza kutekelezwa na Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa hapo tarehe 4 Novemba 2016. Hii ni fursa kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika sera na mikakati ya kuendeleza uchumi wa kijani, utunzaji bora wa mazingira pamoja na upunguzaji wa hewa ya ukaa inayozalishwa hewani.

Bwana Ban Ki-moon anakaza kusema, hata Umoja wa Mataifa uko katika kipindi cha mpito, baada ya Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuridhia uteuzi wa Katibu mkuu wa Tisa wa Umoja wa Mataifa Bwana Bwana Antonio Guterres. Anasema kwamba, amepata heshima kubwa kuwatumikia watu wa Umoja wa Mataifa katika kipindi cha miaka kumi. Kwa pamoja wameweza kuunda misingi ya maendeleo shirikishi yanayopaswa kuendelezwa kwa kuhamasisha zaidi ushiriki wa wanawake, kwa kuwahusisha vijana wa kizazi kipya daima, haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anakiri kwamba, Jumuiya ya Kimataifa katika kipindi cha miaka 10 ya Uongozi wake imeteseka sana kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ambayo imesababisha mateso na mahangaiko makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia huko Mashariki ya Kati, Sudan ya Kusini, Ukanda wa Sahel na sehemu mbali mbali za dunia. Bado kuna vita na athari za majanga asilia ambayo yanaendelea kushughulikiwa kikamilifu na wafanyakazi shupavu wa Umoja wa Mataifa, kazi inayotekelezwa katika mazingira magumu na hatarishi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-moon anapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wote wa Umoja wa Mataifa kwa mchango wao na kwamba, anawataka kutoa ushirikiano wa dhati kwa Katibu mkuu mteule wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa dhamana ya Umoja wa Mataifa katika kulinda na kudumisha amani, maendeleo na haki msingi za binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.