2016-10-24 08:48:00

Kardinali Pengo: Litegemezeni Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa maisha!


Maadhimisho ya Siku ya Kimissionari Duniani ni mwaliko kwa waamini kushikamana kwa pamoja kwa hali na mali, ili kuhakikisha kwamba, Habari Njema ya Wokovu inatangazwa na kushuhudiwa hadi miisho ya dunia. Hii ni dhamana ambayo Wakristo wamejitwalia kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo unaowashirikisha: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo. Katika mapambazuko ya Millenia ya taua ya Ukristo, changamoto kubwa ya Uinjilishaji inajikita kwa namna ya pekee katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam katika mahojiano maalum na Radio Vatican, anakazia umuhimu wa waamini kulitegemeza Kanisa mahalia kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kwa hali na mali, ili kweli huruma na upendo wa Mungu uliofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu, kwa mateso, kifo na ufufuko wake, uweze kuwafikia na kuwaambata wote. Wakristo wasiwe na aibu ya kutangaza na kushuhudia Ukristo wao hata kama itawabidi kugharimika sana!

Ushuhuda unaohimizwa na Mama Kanisa kwa watoto wake anasema Kardinali Pengo ni ile hali ya kuhakikisha kwamba maisha ya waamini yanalandana kwa kiasi kikubwa na maisha ya Yesu Kristo mwenyewe. Hii ni changamoto ya kujitoa bilaya kujibakiza kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Waamini wanapaswa kulitegemeza Kanisa kwa hali na mali. Dhamana hii inawezekana ikiwa kama waamini watajenga utamaduni wa upendo na mshikamano, kwa kila mtu kuchangia kadiri alivyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa kutambua kwamba, kila mtu hata maskini anayo karama ya kuchangia katika ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia!

Nyumba za Parokia na Makanisa Jimbo kuu la Dar es Salaam ni kielelezo hiki cha mshikamano wa upendo katika mchakato wa kulitegemeza Kanisa mahalia kwa njia ya rasilimali watu, vitu na fedha. Kardinali Pengo anapenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza waamini wa Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa majitoleo yao yanayoendelea kulitegemeza Kanisa katika medani mbali mbali za maisha!

Kardinali Pengo anakazia kwa namna ya pekee, ushuhuda wa waamini unaojikita katika mshikamano unaowawezesha kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa. Mshikamano huu unapaswa kupata chimbuko lake katika maisha ya kifamilia, jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, parokia, jimbo hadi kufikia katika Kanisa la kiulimwengu.

Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kujenga na kuimarisha huduma kwa maskini, amani na utulivu kama njia ya kumshuhudia Kristo Yesu, nguvu inayowategemeza wafuasi wake. Waamini waoneshe mshikamano wa umoja, upendo na ukarimuĀ  wakati wa raha na shida, daima wakijitahidi kumwambata Kristo Yesu, aliyeikomboa dunia kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu! Waamini wajitahidi kulifahamu Fumbo la Msalaba na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yao na kamwe wasitafute njia za mkato wanapokumbana na magumu ya maisha kwa kwenda kwa waganga wa kienyeji!

Waamini watambue kwamba, wanaalikwa na Mama Kanisa kushiriki katika mateso yanayokomboa kama ambavyo Mtakatifu Yohane Paulo II anavyolifundisha Kanisa! Huyu ni mtume, shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu, aliyeonja Fumbo la Msalaba hadi dakika ya mwisho wa maisha yake, leo hii Kanisa linamweka mbele ya macho ya waamini kama mfano hai wa kuigwa katika kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.