2016-10-24 07:55:00

Jikiteni kikamilifu katika shughuli za kichungaji na kimissionari!


Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XXX ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, hususan Somo la Pili linamwonesha Mtume Paulo, Mwalimu wa mataifa alipokuwa karibu kuyamimina maisha yake, anayachambua katika hatua kuu tatu, yaani maisha ya sasa, yaliyopita na yale yajayo! Kwa maisha ya sasa Paulo mtume anakaribia kuteswa na kwamba, amevipiga vita vilivyo vizuri katika maisha yake ya nyuma kwa kutekeleza kikamilifu dhamana na utume wake wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu pamoja na kuilinda imani na sasa anapenda kuyakabidhi maisha yake kwa siku za usoni mbele ya Mwenyezi Mungu, hakimu mwenye haki.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 23 Oktoba 2016, uwanja uliokuwa umefurika na bahari ya waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia! Mtume Paulo amefanikiwa katika utume wake, akaonesha haki na kuwa mwaminifu kwa Kristo na Kanisa lake kutokana na nguvu ya Kristo Yesu aliyekuwa pamoja naye, akimsaidia na kumsindikiza ili aweze kuhitimisha kazi ya kutangaza Injili kwa watu wote wa mataifa! Hii ndiyo picha ya Kanisa inayooneshwa na Mtakatifu Paulo, wakati huu wa maadhimisho ya Siku ya 90 ya Kimissionari Duniani, inayoongozwa na kauli mbiu “Kanisa la Kimissionari, shuhuda wa huruma ya Mungu”.

Kwa njia ya Mtume Paulo, Kanisa linapata kielelezo chake, kiasi cha kuliwezesha kutekeleza utume wa Uinjilishaji, changamoto na mwaliko kwa waamini wote kujikita kikamilifu katika shughuli za kichungaji na kimissionari, kwa kutambua kwamba mafanikio ya juhudi hizi si nguvu tu za kibinadamu, bali ni zawadi na nguvu ya Roho Mtakatifu anayeliwezesha Kanisa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake ulimwenguni, hata kama wakati mwingine hakuna mafanikio ya kuridhisha.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, huu ni wakati wa kuonesha ujasiri, ili kuimarisha hatua ya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili; kujipatia imani na nguvu inayofumbatwa katika utume huo. Ni kipindi cha ujasiri ambao haumaanishi mafanikio bali kinawataka waamini kuendeleza mapambano sio kwa nia ya kushinda kwa lazima; kutangaza na wala si lazima kuwaongoa watu.

Ni ujasiri ambao unapania kutoa mwelekeo mpya ulimwenguni bila kinzani wala vurugu. Ni ujasiri unaowataka waamini kuwa wazi kwa watu wote bila kupunguza uelewa wa Kristo kuwa ni Mkombozi wa wote. Ni ujasiri wakupambana na utepetevu wa imani, bila ya kuwa na kiburi, bali kwa kujikita katika fadhila ya unyenyekevu kama aliyokuwa nayo Yule mtoza ushuru anayesimuliwa katika Injili ya siku, ambaye hakuthubutu hata kidogo kuinua macho yake mbinguni, bali alipiga kifua chake kuomba huruma na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hiki ni kipindi cha ujasiri na kwamba, waamini wanapaswa kujivika ujasiri. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Bikira Maria ni kielelezo na mfano wa Kanisa linatoka nje na sikivu kwa Roho Mtakatifu, awasaidie waamini wote kwa nguvu ya Sakramenti ya Ubatizo kuwa kweli ni mitume wamissionari ili kutangaza ujumbe wa wokovu kwa familia nzima ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.