2016-10-24 14:59:00

Acheni unafiki na undumila kuwili katika maisha ya kiroho!


Siku ya Bwana “Dies Domini” ni kumbukumbu ya kazi ya uumbaji iliyofanywa na Mwenyezi Mungu na akapumzika siku ya Saba. Ni Siku ya Kristo, kwa kukumbuka Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo! Ni Siku ya mwanadamu anayopaswa kujipumzisha pamoja na kushiriki na waamini wengine Ibada ya Misa Takatifu tayari kujichotea nguvu na neema ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo katika uhalisia wa maisha. Siku ya kutafakari pia mambo ya nyakati kwa kutenda matendo mema: kiroho na kimwili. Kimsingi huu ni muhtasari wa Waraka wa kichungaji wa Mtakatifu Yohane Paulo II, “Siku ya Bwana” “Dies Domini”.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, Jumatatu, tarehe 24 Oktoba 2015 amegusia jinsi ambavyo Yesu alimponya mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu kwa muda wa miaka kumi na nne, lakini mkuu wa Sinagogi akakasirika kutokana na kitendo hiki cha huruma, kwani alikuwa amevunja Sheria kwa kumponya yule mwanamke siku ya Sabato. Waamini wanaalikwa kuomba neema ya kutembea katika Sheria ya Mungu kwa kuachana na tabia ya unafiki na ugumu wa moyo, hali ambayo mara nyingi inaficha mapungufu ya mtu.

Waamini kamwe wasikubali kuwa ni watumwa wa Sheria, bali wajitahidi kutembea katika uhuru wa watoto wa Mungu, kwani Sheria imewekwa ili kuwasaidia waamini kuwa huru na wana wateule wa Mungu kwa kuondokana na unafiki. Waamini wajenge maisha yao kwenye fadhila ya: upole, utu wema, huruma na msamaha, ili kuondokana na ugonjwa wa kuwa na moyo mgumu hata katika shida na mahangaiko ya wengine. Mara nyingine watu wanaofuata Sheria kwa nguvu wanapenda kuficha udhaifu wao anasema Baba Mtakatifu. Mara nyingi watu hawa si wema, ni wanafiki au ni wagonjwa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mfano wa Baba mwenye huruma unaonesha jinsi ambavyo kijana mkubwa aliyebaki nyumbani kwa Baba yake, akajitahidi kuwa mwema mbele ya Baba yake, lakini hakashindwa kuonesha moyo wa furaha na huruma, mdogo wake aliporejea nyumbani akiwa ametubu na kumwongokea Mungu baada ya kumezwa na malimwengu na huko akakiona cha mtema kuni! Hiki ni kielelezo cha kiburi ambacho kilimfanya kushindwa kutambua na kuonja wema na huruma ya Baba yake. Alikuwa anatembea katika Sheria akiwa na moyo mgumu.

Mwana mpotevu aliitelekeza Sheria, lakini baadaye akatubu na kumwongokea Mungu pamoja na kupata msamaha kutoka kwa Baba mwenye huruma. Si rahisi kutembea katika Sheria ya Bwana, bila kutumbukia katika ugumu wa mioyo anasema Baba Mtakatifu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali ili kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kutembea katika Sheria zake huku wakijitahidi kukita maisha yao katika huruma, upole, utu wema na unyenyekevu, ili wote waweze kutembea katika Sheria ya Bwana, huku wakiongozwa na fadhila hizi katika maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.