2016-10-22 17:15:00

Padre Philippe Alain Mbarga ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Ebolowa


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Sana Padre Philippe Alain Mbarga, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Ebolowa, nchini Cameroon. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Philippe Alain Mbarga alikuwa ni Gombera wa Seminari kuu ya Nkolbisson, iliyoko Jimbo kuu la Yaoundè. Askofu mteule Mbarga alizaliwa tarehe 28 Januari 1968 huko Obout, Jimboni Mbalimayo. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi nchini Cameroon na Ujerumani alikojipatia Shahada ya uzamivu katika somo la Taalimungu Biblia, kunako mwaka 2003.

Itakumbukwa kwamba, alipewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 10 Desemba 1994, kama Padre wa Jimbo Katoliki la Mbalmayo. Tangu wakati huo ameendelea na masomo yake huko Yaounde na Fulda, Ujerumani hadi mwaka 2003 aliporejea nchini mwake na kupewa dhamana ya kufundisha Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika ya Kati. Kuanzia mwaka 2003- 2005 alikuwa Katibu maalum wa Gombera wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika ya Kati.

Mwaka 2005- 2008 akateuliwa kuwa Gombera wa Seminari ya maandalizi na Seminari kuu ya Falsafa ya “Marie Reine de Apòtres” huko Otèlè, Youndè. Kuanzia mwaka 2008 hadi wakati huu alipoteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko alikuwa ni Gombera wa Seminari kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili huko Nkolbison, Youndè.

Askofu mteule Philippe Alain Mbarga alikuwa pia ni Katibu wa Tume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon inayojihusisha na shughuli za kitume. Jimbo la Ebolowa limekuwa wazi tangu tarehe 31 Oktoba 2014 baada ya Baba Mtakatifu Francisko kumhamishia Askofu Jean Mbarga Jimbo kuu la Youndè pamoja na kumpandisha hadhi ya kuwa ni Askofu mkuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.