2016-10-21 15:05:00

Wekezeni zaidi kwa vijana ili kuwajengea matumaini!


Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza wajumbe wa Mfuko wa Yohane Paulo II wakati huu wanapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 30 ya uwepo na utume wao, changamoto ya kuangalia ya mbeleni kwa malengo mapya hususan katika masuala ya elimu, utamaduni, maisha ya kiroho na huduma ya upendo mintarafu karama ya Mtakatifu Yohane Paulo II ambaye Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu yake tarehe 22 Oktoba ya kila mwaka.

Kuna umati mkubwa wa wanafunzi ambao wamefaidika na ufadhili unaotolewa na mfuko huu, kiasi hata cha kuweza kuhitimu masomo yao. Huu ni mwaliko wa kuendeleza kuwekeza hasa kwa vijana wa kizazi kipya, ili waweze kukabiliana na changamoto za maisha huku wakiwa wanafumbata mwanga wa Injili na moyo wa imani. Majiundo kwa vijana ni kitega uchumi kwa siku za usoni, ili kamwe wasipokwe matumaini ya leo na kesho iliyo bora na wajanja wachache!

Baba Mtakatifu Francisko ameyasema haya, Ijumaa tarehe 21 Oktoba 2016 wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa Yohane Paulo II. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yanayoelekea ukingoni imekuwa ni fursa ya kutafakari ukuu wa Huruma ya Mungu katika nyakati hizi ambamo kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, mwanadamu anadhani kwamba, anaweza kujitosheleza kwa kila jambo na kwamba yeye ni muweza wa kila jambo la wala haitaji uwepo na tunza ya Mwenyezi Mungu katika maisha yake.

Kama Wakristo, wanatambua kwamba, utajiri na maweza yote aliyo nayo mwanadamu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, utajiri mkubwa zaidi si fedha na mali ambazo zinaweza kumgeuza mwanadamu kuwa mtumwa, bali ni upendo wa Mungu unaowafanya wote kuwa huru! Baba Mtakatifu bado anakumbuka hija yake ya kitume aliyofanya nchini Poland wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 na kubahatika kuona mahali walikozaliwa mashuhuda na mitume wa huruma ya Mungu: Watakatifu Yohane Paulo II na Sr. Faustina Kowalska.

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Yesu Kristo kwa njia ya maisha na utume wake amewafunulia watu Uso wa huruma ya Mungu inayotenda na kuambata utu wa mwanadamu mzima. Huruma ya Mungu kwa namna ya pekee, inajionesha kwa watu wanaoteseka, katika ukosefu wa haki, katika umaskini pamoja na udhaifu wa kibinadamu unaojionesha kiroho na kimaadili. Kwa upande wake, Mtakatifu Faustina Kowalska anasema anahimizwa na Yesu kuwa na moyo wa huruma unaomwilishwa katika matendo ya huruma, ili kushuhudia na kuwatangazia watu wa mataifa huruma ya Mungu. Ushuhuda wa watakatifu hawa kutoka Poland, iwe ni chachu ya huduma ya upendo na ukarimu inayotekelezwa na Mfuko wa Yohane Paulo II kwa vijana wa kizazi kipya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.