2016-10-21 15:53:00

Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu ni fahari, majivuno na furaha ya Kanisa


Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida, Tanzania katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya uwepo na utume wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu anasema, hii ni Jubilei ya Wamissionari wa C.PP.S., Jimbo Katoliki Singida lakini zaidi ni Jubilei ya Kanisa zima. Wamissionari hawa ni miamba na mashuhuda wa imani, waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwatangazia watanzania Habari Njema ya Wokovu inayojikita katika mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Wamesaidia kupandikiza, kukuza na kudumisha mbegu ya imani ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Singida.

Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania wameshiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa Jimbo Katoliki Singida si tu kwa njia ya huduma zao za kichungaji bali pia katika kulitegemeza Jimbo katika miundo mbali mbali. Kwa hakika wengi wao wamejisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu pasi na kujibakiza, leo hii familia ya Mungu nchini Tanzania inasherehekea matunda ya kazi na jasho la wamissionari hawa.

Kwa njia ya maisha, karama na utume wao, Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, waliyavuta Mashirika mengi ya watawa wa kike kwenda Jimboni Singida ili kushiriki katika utume wa kuwatangazia na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu kwa njia ya huduma ya elimu, afya, maji na maendeleo endelevu. Mashirika ya Watawa wa kike yanaendelea kulitajirisha Jimbo Katoliki la Singida kwa karama na ushuhuda wao wa maisha wenye mashiko na mvuto!

Askofu Edward Mapunda anawapongeza Mapadre wote wanaoadhiisha Miaka 40, 25 na Mwaka mmoja wa Upadre, ili waendelee kujizatiti zaidi katika kuwahudumia watu wa Mungu bila ya kujibakiza kwa kupenda na kuthamini wito na maisha yao ya Kipadre. Mwishoni, Askofu Mapunda anasema, Parokia ya Manyoni, Nyumba mama ya Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu inaadhimisha Jubilei ya miaka 50, changamoto ya kuanzisha Parokia nyingine ili kuendelea kutoa huduma makini kwa familia ya Mungu Jimboni Singida. Ombi hili limetolewa kwa Padre Chesco Msaga mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya Uwepo na utume wa C.PP.S nchini Tanzania. Sherehe hizi zilifanyika hivi karibuni, Parokiani Manyoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.