2016-10-21 08:15:00

Iweni ni mashuhuda wa matumaini na wajenzi wa umoja na mshikamano!


Wanashirika la Mtakatifu Augostino Recolletti wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa matumaini; vyombo na wajenzi wa umoja na mshikamano, ili kuishi kama ndugu wamoja huku wakiwa wameungana: roho moja na moyo mmoja. Hii ndiyo ndoto ya Mtakatifu Augustino inayopaswa kumwilishwa katika nyakati hizi na wanashirika hawa wanapoadhimisha mkutano wao wa 55. Hii ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 20 Oktoba 2016 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wanaoshiriki mkutano mkuu wa Shirika hili hapa mjini Roma.

Baba Mtakatifu amewataka watawa hawa kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini katika mwanga angavu. Wawe kweli ni mashuhuda wanaosimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, tayari kushirikishana karama na mapaji ambayo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yao.

Kuna umati mkubwa wa watu anasema Baba Mtakatifu Francisko wanaowasubiri ili waweze kuwaendea na kwamba, wanawatazama kwa moyo wa upendo ili kuona kile ambacho wanaweza kuwashirikisha watu hao baada ya kukutana na Mwenyezi Mungu. Watawa wahakikishe kwamba, wanatekeleza utashi wa Mungu katika maisha na utume wao badala ya kuendekeza mawazo na miradi yao binafsi. Wawe na ujasiri wa kuambata huruma na upendo wa Mungu, chachu ya mageuzi inayoboresha maisha ya watu. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha mshikamano wa umoja na udugu ili kuondokana na kishawishi cha utengano, kinzani pamoja na ubaguzi na badala yake, amani, umoja, upendo na majadiliano katika ukweli na uwazi vitawale na kukita mizizi yake katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.