2016-10-20 15:44:00

Njia za kumfahamu vyema Yesu: Sala, Ibada, Neno na Toba!


Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni muhtasari wa Imani ya Kanisa, Maadhimisho ya Sakramenti Saba za Kanisa, Maisha adili yanayosimikwa katika Amri kumi za Mungu na mwishoe ni Sala ambayo kimsingi ni mazungumzo kati ya mwamini na Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Alhamisi tarehe 20 Oktoba 2016 amekaza kusema, haitoshi kufahamu Katekisimu yote kama njia ya kufahamu Fumbo la maisha na utume wa Kristo Yesu.

Mwamini kwanza  kabisa anapaswa kujitambua kwamba, ni mdhambi na anahitaji huruma na upendo wa Kristo Yesu sanjari na kuendelea kukuza mahusiano mema na Kristo kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na maadhimisho mbali mbali ya Mafumbo ya Kanisa. Mtakatifu Paulo anawaalika Wakristo wa Efeso kuomba neema ya Roho Mtakatifu katika maisha yao, ili kweli aweze kuwaimarisha na hatimaye, kumwezesha Kristo kuwa ni kiini na kilele cha maisha yao, huku wakimwachia nafasi nyoyoni mwao.

Waamini wanaweza kumfahamu vyema Kristo Yesu kwa kujikita katika maisha ya sala na tafakari ya kina,  kwani ni kwa njia ya Maandiko Matakatifu kwamba, Kristo Yesu amejifunua kwa Watu wa Mataifa, kiasi cha watu kutambua na kuonja pendo lake katika maisha yao. Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa ni fursa makini ya kuendelea kumfahamu Yesu, kwani Katekisimu ya Kanisa Katoliki inampatia mwamini mambo makuu ya imani kwa Kristo na Kanisa lake. Kumbe, hapa kuna haja ya kujenga utamaduni wa kusali bila ya kuchoka kwa kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia kumfahamu Kristo.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kukutana na Kristo Yesu katika ukimya na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu! Waamini wengi wanahitaji kujenga na kudumisha ukimya mtakatifu mbele ya Sakramenti kuu, kwani Kristo Yesu ndiye anayepaswa kuabudiwa na kutukuzwa milele. Waamini watambue pia kwamba, wao ni wadhambi na kwamba, wanahitaji kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, ili kuonja kweli Fumbo la maisha ya Yesu. Kumbe, Sala, Ibada ya Kuabudu, tafakari ya Neno la Mungu, Toba na wongofu wa ndani ni mambo msingi katika safari ya kumfahamu Yesu Kristo, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu baraka hii, ili waweze kumfahamu na hatimaye, kumwambata Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.