2016-10-20 14:57:00

Jubilei ya miaka 50 ya uwepo na utume wa C.PP.S. Tanzania


Wamissionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania linaadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya uwepo na utume wa Shirika hili nchini Tanzania, matunda ya maadhimisho ya Miaka 150 ya uhai wa Shirika ambalo lilianzishwa na Mtakatifu Gaspar del Bufalo kunako mwaka 1815. Katika Makala haya, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inapenda kukushirikisha kwa ufupi: mwanzo, kuenea na karama ya Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu.

Itakumbukwa kwamba, ujio wa Wamissionari wa C.PP.S nchini Tanzania kunako mwaka 1966 lilikuwa ni tunda la Jubilei ya miaka 150 tangu kuanzishwa kwa Shirika. Karama ya Shirika hili inajikita katika utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; Maisha ya Kijumuiya pamoja na kueneza tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu, kielelezo makini cha ufunuo wa huruma ya Mungu kwa binadamu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali duniani.

Kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 yauwepo na utume wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu hivi karibuni nchini Tanzania imekuwa ni fursa ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Mapadri wawili wa kwanza wazalendo ndani ya Shirika yaani Padre Felix Mushobozi na Padre Onesphory Kayombo ambao wanaadhimisha Jubilei ya miaka 25 tangu walipopewa Daraja ya Upadre. Kumbu kumbu hii pia ilipambwa kwa Shemasi Marco Loth kupewa Daraja Takatifu ya Upadre na Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida.

WASIFU NA HISTORIA FUPI YA SHIRIKA – TANZANIA

Mwanzo wa Shirika: Shirika la Wamisonari wa Damu Azizi ni Shirika la Kazi za Kitume la Mapadre na Mabruda lililoanzishwa na Mt. Gaspari del Bufalo tarehe 15 Agosti 1815 huko Giano, Italia, katika Abasia ya Mt. Felix na kuwekwa chini ya Ulinzi wa Mama Bikira Maria na Usimamizi wa Mt. Fransisko Ksaveri. Lengo la Gaspari katika kuanzisha Shirika lilikuwa ni kueneza upendo wa Kristo aliouonesha alipomwaga Damu yake msalabani kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Ndiyo maana Gaspari alisema, “Natamani niwe na ndimi elfu ili upendo huu uwafikie watu wote”.

Kuenea kwa Shirika: Tangu mwanzo huo, maelfu ya Wamisionari wamevutwa na moyo wa Mt. Gaspari na wameendeleza utume huo. Licha ya changamoto nyingi za mwanzoni, Shirika liliendelea kukua hata nje ya Italia. Hadi sasa kuna wanashirika zaidi ya 500 na wameenea katika mabara yote duniani katika nchi zaidi ya 20 zilizogawanyika katika Provinsi 8, Vicariate 4 na Mission 6.

Karama ya Shirika: Wamisionari hawa wanaongozwa na mihimili mitatu: Utume, Maisha ya Jumuiya na Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu. Kwa Gaspari na hata kwa wanashirika wote, Kristo kumwaga Damu yake ilikuwa ni alama ya upendo mkuu wa Mungu kwa watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa (Ufu.5:9; 2Kor.5:14). Tasaufi hii ya Damu Azizi ndiyo inayowahamasisha na kuwasukuma wamisionari waishi pamoja katika jumuiya wakiunganishwa kwa kifungo cha upendo bila kuweka nadhiri, wanapata fursa ya kusali na kutafakari Neno la Mungu ili waende kuhudumia na kuleta upatanisho kati ya watu.

Ujio wa Shirika Tanzania kama tunda la Jubilei ya miaka 150: Makao Makuu ya Shirika hapa Tanzania yalianzia Manyoni, kisha Morogoro na sasa yapo Kisasa, Dodoma (2002). Wanashirika walifika mara ya kwanza Tanzania tarehe 19 Mei, 1966 wakati Shirika lilipokuwa linaadhimisha Jubilei ya miaka 150. Wanashirika watatu: Padre Josefu Montenegro, C.PP.S, Padre Dino Gioia, C.PP.S na Bruda Franco Palumbo, C.PP.S walifika Dodoma na kupokelewa na mapadre Wapassionisti chini ya aliyekuwa Askofu wa Jimbo la Dodoma wakati huo, Mhashamu Askofu Jeremiah Pesce.

Wakati huo Askofu Mattias Isuja Joseph alikuwa Katibu wa Jimbo. Waliwasili Manyoni tarehe 11 Februari 1967 na kuanza rasmi kuwahudumia watu wa Manyoni na vitongoji vyake; wakati huo ikiwa katika Jimbo la Dodoma. Kwa kipindi cha miezi kadhaa kabla ya kukabidhiwa shughuli za kitume wilayani Manyoni, Wamisionari hao waliishi Jimboni Dodoma. Padre Kandido mwanashirika wa Shirika la Mateso Jimboni Dodoma alikuwa kiongozi wao katika kipindi cha kujiandaa kufanya kazi za kimisionari hapa Tanzania.

Wenyeji waliowapokea wamisionari wa kwanza Manyoni ni pamoja na Lazaro Kayombo – aliyekuwa mfanyakazi wa reli, Katekista Roman Mwinyipanduka, Hilary Msahala – aliyekuwa mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Manyoni, Thadei Mhagama – aliyekuwa msaidizi wa Mkuu wa Magereza - Gereza la Manyoni, Julitha Mtonyi na mume wake – wakulima, Moses Chambago, Maria – ambaye baadaye alikuwa mpishi wa mapadre, Paulo Mwimbwa – baadaye akawa katekista na Mwalimu Floriani.

Wamisionari wengine waliofika baadaye kufanya kazi Tanzania ni pamoja na Fr. Mario Dariozzi, Br. Umberto Reale, Fr. Domenico Altieri, Fr. Vincent Boselli, Br. Antony Canterucci, Fr. Francis Bartoloni, Fr. Ernesto Gizzi, Fr. John Piepoli, Fr. Sebastian Benedettini, Fr. Antonio Kalabrese, Fr. Enzo Zoino, Fr. Gennaro Cespites, Fr. Mario Brotini, Fr. Cosimo Turi, Fr. Timothy Coday, Fr. Brendan Dohertry, Br. Alan na Fr. James Froelich. Mwaka 1969, masista wanne Waabuduo Damu ya Kristo kutoka Italia (Sr. Delphina Gnere, Sr. Angelina Palmigiani, Sr. Nicolina Scataglia na Sr. Romana Sacchetti) walifika Tanzania na kuanza kushirikiana na Wamisionari hawa katika kueneza Neno la Mungu na huduma za kijamii.

Utume: Tangu mwanzoni, wamisionari waliweka mkazo kwenye utume wa Kanisa kwa mataifa, wakihubiri Neno la Mungu kwa watu wote na kubatiza wanaoamini. Wanaeneza Neno la Mungu kwa njia mbali mbali, huduma maparokiani, mafungo ya kiroho, utume kwa vijana, huduma za jamii kama hospitali, shule, maji na maendeleo mbali mbali ya jamii.

Baada ya kufungua nyumba ya Manyoni na kwa kusoma alama za nyakati, kutokana na ongezeko la waaamini na wahitaji, wamisionari kwa kushirikiana na Askofu Bernad Mabula, walifungua Parokia ya Itigi (1973) na baadaye Chibumagwa (1978) katika Jimbo la Singida. Kwa vile wamisionari hawa walihitaji vitu mbalimbali kutoka Dar es Salaam iliwalazimu kufungua nyumba ya Procura na hatimaye Baba Kardinali Laureani Rugambwa aliwaomba wafungue Parokia ya Tegeta (1979) Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Ongezeko la waamini lililazimu kufungua Parokia nyingine ikiwemo Parokia ya Mt. Nicholaus, Kunduchi Mtongani (1999) na baadaye Kituo cha Hija na Parokia ya Mt. Gaspar Del Bufalo Mbezi Beach (2007). Hata hivyo leo kuna Parokia ya Mwenyeheri Isdori Bakanja, Boko (2003) na Parokia ya Mt. Andrea Mtume - Bahari Beach (26 Agosti 2012) katika Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam. Katika Jimbo la Morogoro Shirika linahudumia Parokia ya Mwili na Damu - Kola B (2002); Jimbo la Ifakara wanashirika wapo katika Parokia ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume – Mkula (Oktoba 2007); Jimbo la Dodoma Parokia ya Bikira Maria Mama wa Damu Azizi, Kisasa (2 Januari 2011) na Parokia ya Mt Fransisko Ksaveri ya Chuo Kikuu cha Dodoma - UDOM (19 Disemba 2015).

Taasisi nyingine zilizoanzishwa kama sehemu ya utume wa Shirika ni pamoja na Manyoni VTC (1973/74), St. Gaspar Hospital - Itigi (15 Mei 1989), C.PP.S Water Project – Atlantic Province (1975), St. Gaspar VTC - Mtongani [...], Radio Mwangaza (24 Disemba 2002), St. Gaspar Hotel and Conference Centre (2010), St. Gaspar Nursing School [...], Mission Development Foundation – MDF [...] na Gaspar del Bufalo House – GdB House, Tegeta (6 Julai 2016).

Licha ya utume wa kawaida wa Neno la Mungu na huduma za kijamii, Shirika limekuwa mstari wa mbele kuwashirikisha watu mmoja mmoja na katika vikundi karama yake. Vipo vikundi vyenye majina mbali mbali karibu mahala pote wanapofanya kazi wamisionari, lakini kwa pamoja vinajulikana kama “Utume wa Damu” wakishirikiana na wale waliowahi kupata malezi ya kishirika (Ex-Seminarians). Mahusiano ya vikundi hivi na Shirika yanawasaidia watu waendelee kukua kiroho na kupata fursa ya kushiriki utume wa Shirika kila mmoja kadiri ya karama na nafasi.

Malezi na Waseminari: Wamisionari walitamani utume wa Shirika hapa Tanzania uwe endelevu. Baada ya miaka kadhaa ya uzoefu wa mazingira, mila na tamaduni za kitanzania, walianzisha kazi ya malezi kwa vijana walioonesha nia ya kujiunga na Shirika. Walijenga Nyumba ya Kwanza ya Malezi ya Mt. Fransisko Ksaveri, Itigi, baadaye Nyumba ya Mtumishi wa Mungu John Merlini, Miyuji – Dodoma na hatimaye St. Gaspar College, Morogoro. Kwa sasa Shirika lina waseminari zaidi 60 walio katika ngazi mbali mbali za malezi. Wamisionari wa kwanza wazalendo, Fr. Felix Mushobozi na Fr. Onesphory Kayombo ambao wanasherehekea jubilei ya fedha ya upadre, walipatikana mwaka 1990. Tangu wakati huo idadi ya wamisionari imeongezeka hadi kufikia 75 mwaka huu.

Ushirikiano na Provinsi nyingine za Shirika: Provinsi ya Tanzania ni sehemu ya Shirika zima duniani na hivyo maisha na utume wake ni sehemu ya utume wa Shirika zima. Tanzania imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na wanashirika wengine mahali pengine duniani, mfano, Provinsi za Italia, Atlantic (Kanada), Iberia (Hispania, Ureno na Guinea Bissau), Kansas City na Cincinnati (Amerika Kaskazini na Kusini), Teutonic (Ujerumani na Austria), Poland na Vikarieti ya India. Provinsi imekuwa tayari kuwatuma wamisionari wake mahali pengine na kupokea wamisionari kutoka Provinsi nyingine za Shirika kushiriki utume wake. 

Ukuaji wa Shirika: Idadi ya wamisionari iliongezeka, utume wa Shirika ulipanuka, Shirika hapa Tanzania limeendelea kukua hadi kufikia ngazi ya Vikarieti mwaka 1998 na hatimaye ngazi ya Provinsi tarehe 8 Agosti 2015 kama tunda na zawadi ya Jubilei ya miaka 200 ya uhai wa Shirika. Mapadre waliowahi kuongoza Shirika hapa Tanzania kwa nyakati tofauti ni Fr. Dino Gioia, Fr. Francis Bartoloni, Fr. Antonio Kalabrese, Fr. Vincent Boselli, Fr. Joachim Ndelianaruwa, Fr. Reginald Mrosso na Fr. Chesco Msaga. Hata hivyo, kwa kipindi cha miaka 50, Shirika hapa Tanzania limekuwa na changamoto nyingi pamoja na kuwapoteza wapendwa wake sita kwa nyakati tofauti; Fr. Antonio Kalabrese, Fr. Basil Ndeshingio, Fr. Joachim Ndelianaruwa, Fr. Ansovinus Makwanda, Fr. Fabian Ruganyiza na Fr. Ernesto Gizzi aliyefariki tarehe 14 Agosti 2016 huko Albano, Italia. Raha ya milele uwape Ee Bwana ...

HITIMISHO: Tunamshukuru Mungu kwa wema wake, Mt. Gaspari Mwanzilishi wetu, Bikira Maria Mama wa Damu Azizi na Mt Fransisko Ksaveri Msimamizi wetu. Tunawashukuru wamisionari wote wa Shirika, Maaskofu, Mapadre, Watawa, wafadhili, watu wote tunaofanya nao kazi na wote wenye mapenzi mema. Siku hii ya jubilei ya miaka 50 ya uwepo wa Shirika Tanzania, miaka 25 ya upadre wa Fr. Felix Mushobozi na Fr. Onesphory Kayombo na upadrisho wa Fr. Marco Raphael Loth iwe ni chachu kwetu sote ya kufanya tathmini ya kweli katika maisha yetu ya kimisionary kwa lengo la kuyaboresha zaidi, kutambua alama za nyakati ili kujibu vema mahitaji ya watu wa sasa kadiri ya mazingira yetu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.