2016-10-20 09:44:00

Jubilei ya miaka 300 ya Bikira Maria wa Aparecida, Brazil


Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil limezindua rasmi maadhimisho ya Jubilei ya Bikira Maria wa Aparecida kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 300 tangu Sanamu ya Bikira Maria wa Aparecida ilipookotwa mtoni kunako mwaka 1717. Hii ni fursa anasema Askofu mkuu Josè Antònio Aparecido Tosi Marques. Ibada kwa Bikira Maria miongoni mwa wananchi wa Brazil ina chimbuko lake katika mapambano dhidi ya ukoloni wa Wareno uliowawezesha wamissionari wakati wa machakato wa Uinjilishaji kujenga makanisa mengi yaliyowekwa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Sanamu ya Bikira Maria wa Aparecida iliokotwa na wavuvi watatu ambao walikesha usiku kucha wakivua samaki, lakini wakaambulia patupu!

Baadaye, wakavua Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili na huo ukawa ni mwanzo wa mafanikio makubwa katika shughuli zao za uvuvi, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Bikira Maria kwa watoto wake wanaopambana na hali ngumu ya maisha pamoja na umaskini! Kunako mwaka 1983 Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil likajenga Kanisa kuu la Bikira Maria wa Aparecida linalopokea idadi kubwa ya mahujaji kutoka ndani na nje ya Brazil, wanaokwenda kutoa heshima zao kwa Bikira Maria Mama wa huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2013 yaliyofanyika nchini Brazil aliitaka familia ya Mungu nchini Brazil, kuendeleza kumbu kumbu hii kama sehemu ya mchakato wa hija ya wananchi wa Brazil kutaka kukutana na Mwenyezi Mungu anayewafunulia waja wake uso wa huruma, hata katika umaskini wao, kwa njia ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kama alivyofanya wakati wa maadhimisho ya Arusi ya Kanisa, alipomwambia Yesu, hawana divai!

Maadhimisho haya yanalenga kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa familia ya Mungu nchini Brazil dhidi ya ubaguzi na nyanyaso zinazoweza kujikita katika ukabila na rangi ya mtu. Malkia Isabela D’Orleans-Braganza aliguswa kwa namna ya pekee na Ibada kwa Bikira Maria kiasi kwamba, akawa nikati ya watu waliosimama kidete kupambana na hatimaye kufutwa kwa biashara ya utumwa, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu, kwa kumwachia nafasi Bikira Maria ili aweze kusaidia mchakato wa uponyaji kutokana na madhara ya biashara ya utumwa nchini Brazill.

Bikira Maria wa Aparecida ni kielelezo cha Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Jubilei ya Bikira Maria wa Aparecida ni changamoto kwa familia ya Mungu nchini Brazil kujikita zaidi na zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo wenye mvuto na mashiko! Ni kipindi cha neema, umoja na udugu na mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Askofu mkuu  Josè Antònio Aparecido Tosi Marques anaadhimisha pia Jubilei ya miaka 25 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu, zawadi ya Mama yake mzazi kwa Bikira Maria wa Aparecido, chemchemi ya Ibada kwa Bikira Maria katika familia yake. Anasema, alizaliwa tarehe 13 Mei, Siku kuu ya Bikira Maria wa Fatima na wazazi wake walifunga ndoa tarehe 8 Desemba, Sherehe ya Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili. Tangu utotoni mwake, ameonja ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Matukio yote haya yawasaidie waamini kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, juhudi ambazo zilifanywa kwa namna ya pekee kabisa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake. Bikira Maria wa Aparecida, aiombee familia ya Mungu nchini Brazil ili iwe kweli shule ya umoja, udugu na mapendo ya kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.