2016-10-19 15:32:00

Mwambateni Kristo Yesu, ili kuwatumikia vyema watu wa Mungu!


Maadhimisho ya Siku kuu ya Mwinjili Luka sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu hapo tarehe 18 Oktoba 2016 ni matukio ambayo yamepamba ufunguzi wa Mwaka wa masomo 2016 – 2017 wa Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, tukio ambalo limetanguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Leondardo Sandri na Padre Arturo Sosa, Mkuu wa Wayesuit akatoa mahubiri. Kanisa limemwombea heri na baraka katika maisha na utume wake kama kiongozi mkuu wa Shirika la Wayesuit.

Kwa upande wake, Kardinali Sandri katika hotuba yake amekazia umuhimu wa kupyaisha maisha yao yote ili kumwambata Kristo Yesu, ufunuo wa huruma ya Mungu, tayari kuwahudumia watu wa Mungu kwa njia ya maisha adili na matakatifu yanayompendeza Mwenyezi Mungu. Wakleri na watawa waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu.

Katika mwelekeo huu, Kardinali Sandri amewataka kujikita zaidi katika ujumbe unaotolewa na Mwinjili Luka katika Injili yake inayoelekezwa kwa watu wa mataifa kwa kuonesha: Umuhimu wa Fumbo la Umwilisho kama kielelezo makini cha uwepo wa Mungu katika maisha na historia ya binadamu. Huyu ni Mungu anayefunua utukufu wake katika hali ya unyenyekevu, kama Mwanga wa Mataifa. Mwinjili Luka kwa namna ya pekee anakazia huruma na upendo wa Mungu unaojifunua kwa maskini, wagonjwa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; mafundisho makuu yanayoonekana kwa namna ya pekee katika mifano ya huruma ya Mungu kwa binadamu.

Hii inaonesha utashi wa Mungu kutaka kumkomboa mwanadamu na hatimaye kumwonesha na kumshirikisha maisha ya uzima wa milele. Kardinali Sandri anasema hapa mambo msingi ni: Fumbo la Umwilisho, Huruma ya Mungu na Hamu ya Mungu kwa binadamu. Majiundo na elimu inayotolewa katika Taasisi hii ya kipapa inapaswa kuwa na mwelekeo wa kimataifa ili kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa la kiulimwengu.

Baba Mtakatifu Francisko anatambua na kuthamini mchango unaotolewa na Taasisi hii ndiyo maana amekubali kushiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki katika tarehe itakayopangwa. Hapa kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi kuhusu dhamana na wajibu wa Taasisi hii katika kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene, umoja na mshikamano katika medani mbali mbali za maisha.

Wasomi kutoka Makanisa ya Mashariki wanapaswa pia kuchangia kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu, hasa kwa kutoa tafakari kuhusu Nyaraka mbali mbali zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa mwono wa Kimashariki. Umuhimu wa Sinodi katika Millenia ya Kwanza ya Ukristo ni Waraka muhimu sana katika kukuza mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Wakristo na Waorthodox; mahusiano ambayo yanapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waaamini. Wasomi wawe na ujasiri wa kufanya rejea katika machapisho mbali mbali ya Mababa wa Kanisa kwani yanafumbata utajiri mkubwa ndani mwake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.