2016-10-19 11:11:00

Chakula na maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu!


Kuwalisha wenye njaa na kuwanywesha wenye kiu ni sehemu ya matendo ya huruma kimwili, ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameitafakari wakati wa katekesi yake, Siku ya Jumatano, tarehe 19 Oktoba 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Haya ni matendo ambayo yanawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuguswa na mahangaiko ya mamillioni ya watu wanaoteseka na kufa kutoka na baa la njaa na ukosefu wa maji safi na salama na kwamba, waathirika wakubwa ni watoto wadogo.

Baba Mtakatifu katika katekesi yake wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga moyo na utamaduni wa upendo na ukarimu kwa maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa jamii kwa kujihusisha kikamilifu badala ya kuwapatia kisogo na kuwabeza. Waamini wanaposali Sala kuu ya Baba Yetu, watafakari kwa kina ombi la chakula cha kila siku wanalolitoa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwa uchungu mkali kwamba, baa la njaa ni mateso makali katika maisha ya mwanadamu. Watu walioshi nyakati za vita au wakati wa ukame wanatambua makali ya baa la njaa. Lakini, jambo la kusikitisha ni kuona kamba, kuna baadhi ya watu wanakula, wanashiba, wanasaza na kutupa chakula, badala ya kutoa chakula hiki ili kuwasaidia maskini na watu wanaoteseka kwa baa la njaa!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwilisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili na leo kwa namna ya pekee kwa kuwalisha wenye njaa na kuwanywesha wenye kiu, kielelezo cha imani tendaji! Waamini wajenge utamaduni wa kusikiliza na kuwahudumia wengine katika mahitaji yao: kiroho na kimwili! Baba Mtakatifu anaendelea kusema kuwa hata Yesu katika maisha na utume wake, alionesha huruma kwa kuguswa na mahangaiko ya watu waliokuwa wanamfuasa siku nzima bila kupata chakula!

Badala ya kuwatawanya kila mtu aende mjini kujitafutia chakula, aliwataka Mitume wake wawapatie chakula, kwa kubariki na kuigawa ile mikate mitano na samaki wawili, maelfu ya watu wakala na kushiba, hapa wafuasi wa Yesu wakajifunza kumtumainia Mwenyezi Mungu na kugawana hata kile kidogo walichokuwa nacho kwa moyo wa ukarimu na mapendo! Huu ni mwaliko wa kushirikishana zawadi ya imani inayogeuka kuwa ni utajiri mkubwa kupita kiasi!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuwalisha wenye njaa na kuwanywesha wenye kiu ni dhamana ya kimaadili kwa Kanisa la Kiulimwengu. Chakula na maji ni kati ya haki msingi za binadamu na haki nyingine zote zinapata umuhimu wake katika: Chakula na Maji, changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga moyo wa upendo na mshikamano wa dhati ili kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata chakula na maji safi na salama kwa ajili ya matumizi yao kama sehemu ya haki msingi za binadamu pasi na ubaguzi. Yesu mwenyewe anasema kwamba, Yeye ni mkate wa uzima wa milele na anapenda kuwaalika wote wenye njaa na kiu kujongea mbele yake ili aweze kuwalisha na kuwanywesha. Matendo haya ya huruma kimwili, yanajenga uhusiano na Mwenyezi Mungu ambaye amejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, Uso wa huruma!

Baba Mtakatifu katika salam na matashi mema kwa mahujaji na wageni waliohudhuria Katekesi yake, ametambua uwepo wa wageni kutoka Ghana, Uganda na Afrika ya Kusini pamoja na kuwatakia wote neema na upyaisho wa maisha ya kiroho katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Fursa ya kukutana na kuzungumza na Khalifa wa Mtakatifu Petro iwe ni changamoto ya kuwa kweli ni mashuhuda amini wa Kristo na Kanisa lake, kwa njia ya imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Waamini wajenge utamaduni wa upendo na mshikamano na maskini wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku! Waamini wajitahidi kushinda ubaya kwa kutenda mema! Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko amekumbusha kwamba, Jumapili ijayo tarehe 23 Oktoba 2016, Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya Kimissionari Duniani, fursa adhimu ya kutafakari kuhusu mchakato wa kuendeleza dhamana na utume wa kimissionari ndani ya Kanisa na kwa kila Mkristo. Kila mwamini anahamasishwa kuwa ni chombo cha kimissionari kwa Kuinjilisha maeneo wanamoishi na kufanya kazi. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaweka waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba, ambaye Kanisa linafanya kumbu kumbu yake kila mwaka, ifikapo tarehe 19 Oktoba!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.