2016-10-18 15:17:00

Washindi wa Tuzo ya Joseph Ratzinger kwa mwaka 2016


Mfuko wa Joseph Ratzinger, Baba Mtakatatifu Mstaafu Benedikto XVI, umetangaza Washindi wa Tuzo ya Ratzinger kwa mwaka 2016 itakayotolewa mjini Vatican hapo tarehe 26 Novemba 2016 ni: Monsinyo Inos Biffi, Jaalim na mwanataalimungu mahiri katika uwanja wa kimataifa na mwandishi mashuhuri wa vitabu na majarida kadhaa. Amezawadiwa tuzo hii kutokana na mchango wake katika masuala ya kitaalimungu na kifalsafa nyakati za kati!

Msomi mwingine ni Ioannis Kourempeles, mwamini wa Kanisa la Kiorthodox, Jaalim wa taalimungu Chuo kikuu cha Aristotle huko Thesalonike, nchini Ugiriki. Tuzo hii inayotolewa na Mfuko wa Joseph Ratzinger, Baba Mtakatatifu Mstaafu Benedikto XVI inapania kuonesha moyo wa shukrani kutoka kwa Mama Kanisa kwa watu wanaojipambanua kutokana na mchango wao katika kazi, maisha na tafiti zinazolisaidia Kanisa kuwafunda watu mbali mbali kutokana na kazi na machapisho yao ya kisayansi. Tuzo hii inapenda kuwahamasisha wasomi kusaidia mchakato wa Mama Kanisa katika kuwarithisha watu wa kizazi hiki ujuzi na maarifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.