2016-10-18 10:47:00

Kongamano la kimataifa kuhusu wito wa Kipadre!


Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri kuanzia tarehe 19 - 21 Oktoba 2016 linaendesha Kongamano la Kimataifa kuhusu Miito linaloongozwa na kauli mbiu “Akamwangalia kwa huruma, akamchagua” “Miserando atque eligendo”. Hali ya miito ya Kipadre, Mafundisho Tanzu ya Kanisa kuhusu miito, Utume wa Kikasisi na Shughuli za kichungaji kwa ajili ya miito ni kati ya mada zitakazochambuliwa kwa kina na mapana wakati wa kongamano hili.

Kongamano hili ni muhimu sana wakati huu Mama Kanisa anapoangalia namna bora zaidi ya kufundisha na kurithisha imani na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na kuwasaidia kung’amua na kutambua mapenzi ya Mungu katika maisha yao, ili vijana waweze kuwa na ujasiri wa kujitosa kimasomaso bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtumikia Mungu na jirani zao.

Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri atatoa hotuba elekezi kwa ajili ya maadhimisho ya kongamano hili, litakalofafanuliwa kwa kina na Makatibu wakuu na baadaye, Kardinali Alberto Suàrez Inda kutoka Mexico atawasilisha mada kuhusu shughuli za kichungaji kwa ajili ya miito ndani ya Kanisa. Dr. Bruna Costacurta atazungumzia kuhusu motisha ya maisha ya kiroho: Huruma ya Mungu na wito ndani ya Biblia. Siku ya kwanza itafungwa kwa Masifu ya Sala ya Jioni.

Alhamisi, tarehe 20 Oktoba 2016, Kardinali Alberto Suàrez Inda ataongoza Ibada ya Misa Takatifu na baadaye Askofu mkuu Benvenuto Italo Castellani atachambua hali ya miito ndani ya Kanisa. Padre Amadeo Cencini atafanua kwa kina na mapana mambo yanayojiri katika masuala ya miito ndani ya Kanisa. Bwana Dante Vannini ataelezea mwelekeo wa kimataifa mintarafu miito. Jioni, wajumbe wa kongamano hili watajikita zaidi katika: Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu miito! Kardinali Vincent Gerald Nichols atatoa muhtasari wa mafundisho ya Mama Kanisa kuhusu miito ndani ya Kanisa, baadaye wajumbe watabadilishana uzoefu na mang’amuzi yao kuhusiana na miito. Wajumbe wataifunga siku kwa Sala ya Jioni, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na taarifa ya makundi ya wajumbe wa kongamano hili.

Ijumaa, tarehe 21 Oktoba 2016, wajumbe wataadhimisha Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu kwa kupitia Lango la huruma na baadaye kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican itakayoongozwa na Kardinali Beniamino Stella. Baadaye, watakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Jioni wajumbe watapata fursa ya kupembua kwa kina na mapana Utume wa Kikasisi na Shughuli za kichungaji kwa kuangalia utamaduni wa miito kwa Makanisa mahalia, tema itakayowasilishwa na Askofu msaidizi Milton Luis Troccoli Cebeido.

Kwa upande wake, Askofu msaidizi Aliaksandr Yasheuski atajadili kuhusu dhamana ya wachungaji mintarafu miito wakati Askofu Gualtiero Sigismondi atachambua kuhusu utunzaji na uchaguzi wa miito ya Kipadre na hatimaye, Kardinali Beniamino Stella atakunja jamvi la maadhimisho ya kongamano la miito linalopania kulipatia Kanisa watenda kazi wema, wachapakazi na watakatifu, watakaoishi na kutenda kadiri ya Yesu Kristo mchungaji mwema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.