2016-10-17 10:01:00

Umuhimu wa dini kushirikiana ili kukabiliana na changamoto mamboleo!


Wakristo na Wadaoisti wanapaswa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kwa pamoja waweze kujizatiti kutafuta ukweli na kushirikiana katika huduma kwa maskini pasi na ubaguzi, ili hatimaye, kuondokana na ubaguzi na hali ya kutoelewana na kuthaminiana kati ya waamini wa dini hizi mbili! Waamini wanapaswa kusimama kidete ili kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo; mshikamano, umoja na udugu.

Waamini wa dini hizi mbili wanapaswa kushikamana na kushirikiana ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Waamini wajenge ari na moyo wa sala mintarafu moyo wa sala kwa ajili ya kuombea amani iliyofanyika mjini Assisi. Haya ni mambo makuu ambayo yamebainishwa na Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, Ijumaa tarehe 14 Oktoba 2016 wakati alipokuwa anashiriki katika majadiliano ya kidini.

Majadiliano haya yameongozwa na kauli mbiu “Kutafuta ukweli kwa pamoja: Majadiliano: Wakristo na Wadaoisti”. Majadiliano haya yaliandaliwa na “Taipei Baoan Temple Foundation” kutoka Taiwan kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini pamoja na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, Baraza la Maaskofu la Kanda ya Maaskofu Katoliki China na Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Majadiliano haya ya kidini yamefanyika miezi michache tu tangu Baba Mtakatifu Francisko, hapo tarehe 20 Septemba 2016 alipokwenda mjini Assisi kwenda kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani. Wakati ule aliwaomba waamini wa dini mbali mbali pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani na kwamba, amani ni matunda ya majadiliano ya kidini yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; ustawi na maendeleo ya wengi.

Mchakato wa kutafuta ukweli kwa pamoja hauwezi kuondoa tofauti zilizoko kati ya dini mbali mbali duniani na kwamba, Kanisa Katoliki haliyakatai yoyote yaliyo ya kweli na matakatifu katika dini mbali mbali duniani. Kanisa linaheshimu namna ya kutenda na kuishi kwa kuzingatia mwanga wa Ukweli unaomwangazia kila mwamini. Itakumbukwa kwamba, dini zina utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho na tunu msingi katika maisha ya kiutu. Majadiliano ya kidini yamehitimishwa rasmi tarehe 17 Oktoba 2016.

Askofu Ayuso anasema, huu umekuwa ni wakari wa kushuhudia imani katika hali ya unyenyekevu, ili kwa pamoja waweze kugundua utajiri unaofumbatwa katika maisha ya kiroho, tayari kujibu changamoto mamboleo zinazomwandama mwanadamu katika nyakati hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni wajibu wa waamini wa dini mbali mbali kuutafuta na kuumbata Ukweli wa maisha, ili kukabiliana na changamoto zinazojikita katika vita, misimamo mikali ya kiimani, chuki na uhasama, tayari kutembea katika hija ya pamoja katika haki na ukweli ili kujenga dunia ambamo misingi ya udugu na mshikamano vinatawala katika akili na nyoyo za watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.