2016-10-17 14:58:00

Miaka 25 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Slovenia


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 17 Oktoba 2016 amekutana na kuzungumza na Rais Borut Pahor wa Jamhuri ya Watu wa Slovenia, ambaye baadaye amekutana pia na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameandamana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo yao ya faragha, viongozi hawa wawili wameonesha kuridhishwa na mahusiano mazuri kati ya nchi hizi mbili, hasa wakati huu nchi hizi zinapojiandaa kuadhimisha Jubilei ya miaka 25 ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na Slovenia. Baba Mtakatifu na mgeni wake, wamegusia masuala yanayogusa hali halisi ya nchi ya Slovenia na baadaye wakajikita zaidi kuhusu uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na Serikali.

Wamekazia umuhimu wa kuendeleza mchakato wa majadiliano na ushirikiano wa dhati kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wengi wa Slovenia, lakini zaidi kwa ajili ya mafao ya vijana wa kizazi kipya. Mwishoni, viongozi hawa wamejadili kwa kina na mapana hali ya kimataifa kwa kujielekeza zaidi katika changamoto zinazojitokeza katika Ukanda huo na kwa Bara la Ulaya katika ujumla wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.