2016-10-16 14:04:00

Wayesuit watakiwa kusimama kidete kupambana na changamoto mamboleo!


Padre Arturo Sosa, Mkuu wa Shirika la Wayesuit aliyechaguliwa hivi karibuni, Jumamosi tarehe 15 Oktoba 2016 ameadhimisha Ibada ya Misa ya shukrani, huku akiungana na wajumbe wa mkutano mkuu wa thelathini na sita wa Shirika la Wayesuit kumtolea Mungu sifa na shukrani kwa hatua hii ya kwanza katika mkutano wao, chemchemi ya imani na matumaini ya Shirika kwa sasa na kwa siku za usoni! Katika mahubiri yake, amewataka Wayesuit kuwa mashuhuda amini wa imani katika ulimwengu mamboleo.

Padre Sosa amewataka Wayesuit kusimama kidete kulinda, kuliendeleza na kulidumisha Shirika lao ambalo kimsingi si kazi tu ya mikono ya wanadamu, ambayo inaweza kuliendeleza, lakini zaidi ni kwa mkono na nguvu wa Yesu Kristo, msingi wa matumaini yao. Huu ni mwaliko wa kulidumisha Shirika kwa njia ya maisha ya kiroho, mchango unaopaswa kutolewa na kila mwanashirika, jumuiya na wale wote wanaoishi na kushirikishwa utume na karama ya Wayesuit sehemu mbali mbali za dunia.

Katika mwelekeo huu, Wayesuit pia wanapaswa kunoa akili na vichwa vyao kwa kukuza na kudumisha kipaji cha ugunduzi ili kushiriki kikamilifu zaidi katika utume wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu mintarafu karama na maongozi ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, mwanzilishi wa Shirika lao. Wawe ni wepezi wa kusoma alama za nyakati ili kugundua changamoto zinazomkabili binadamu katika mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini, ukosefu wa usawa na haki msingi za binadamu; dhuluma na nyanyaso.

Wayesuit wawe mstari wa mbele katika kukoleza uelewa wa kitaalimungu sanjari na kuisaidia familia ya Mungu kuwa imani thabiti, paji ambalo wanapaswa wao pia kumwomba Kristo Yesu, ili aweze kuwakirimia. Padre Sosa anasema, uongozi wa awamu hii unapenda kujielekeza zaidi katika kukuza na kudumisha mahusiano na ushirikiano na watu wengi zaidi, ndani na nje ya Kanisa, ili kushirikishana mang’amuzi ya uzoefu wa uwepo wa Mungu katika hija ya maisha ya mwanadamu, kwani kuna watu wengi ambao wameitwa na kutumwa kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu duniani, dhamana ambayo wanashirikiana pia na watawa wa mashirika mengine ya kitawa na kazi za kitume.

Ni kwa njia ya ushirikiano na mshikamano makini na wenye mashiko, Wayesuit wataweza kukuza na kukoleza miito ya maisha matakatifu miongoni mwa vijana wa kizazi kipya wanaotamani kushiriki maisha na utume wa Wayesuit duniani. Dhamana hii inatekelezwa kwa njia ya sala, majiundo makini na endelevu kwa vijana wanaotaka kujiunga na Shirika. Vijana hawa wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo amini vya utajiri wa tamaduni na watu wa mataifa mbali mbali walioenea kwenye uso wa dunia; watu ambao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.