2016-10-16 09:56:00

Shuhudieni utandawazi wa utakatifu wa maisha ya Kikristo!


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu anasema, wenyeheri: Solomon Leclercq, mtawa na shahidi; Josè Sànchez de Riò, mlei na shahidi; Manuel Gonzàlez Garcìa, Askofu na muasisi wa Umoja wa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na Shirika la Watawa Missionari wa Ekaristi Takatifu wa Nazareth; Alfonso Maria Fusco, Padre na mwanzilishi wa Shirika la Watawa wa Mtakatifu Yohane Mbatizaji, Ludovico Pavoni, Padre na mwanzilishi wa Shirika la Watawa Watoto wa Bikira Maria Immakulata; Josè Gabriel del Rosario Brochero, Padre pamoja na Sr. Elizabeth Catez ni waamini wanaonesha na kushuhudia utandawazi wa utakatifu ndani ya Kanisa.

Maisha ya utakatifu hayaangalii sura, mahali anapotoka mtu, kabila au utaifa wake na kwamba, waamini wote wanaalikwa na Mama Kanisa kuwa ni watakatifu, kwa kumshuhudia KristoYesu kwa njia ya maisha yenye mashiko na mvuto, hata ikiwabidi kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Wenyeheri saba waliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 16 Oktoba 2016 kuwa Watakatifu ni mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu na vyombo vya huruma ya Mungu inayojikita katika uhalisia wa maisha yao.

Utakatifu huu unafumbatwa kwa namna ya pekee katika: Toba, msamaha na upatanisho; Ukarimu, sadaka na huruma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Haya ni mambo makuu yanayowapambanua watakatifu wapya waliotangazwa na Mama Kanisa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma, kila mwamini anayo karama ya kushirikisha katika mchakato wa ushuhuda wa maisha matakatifu kama: Mlei, Mtawa na Padre.

Hawa ni watu ambao walijifungamanisha na Kristo Yesu katika maisha yao, wakawa kweli ni majembe ya imani, matumaini, huruma na mapendo ya Mungu kwa watu wa nyakati zao. Ni maabara ya Ukristo mpya unaotambua na kuthamini tamaduni za watu mahalia, kwa kuzisafisha na kuzitakatifuza tamaduni zile zinazopingana na tunu msingi za Kiinjili. Hivi ndivyo watakatifu wengi walivyoishi na kumshuhudia Kristo Yesu katika maeneo yao, huku wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Kardinali Angelo Amato anaendelea kusema, Mtakatifu Solomon Leclercq, Shahidi alijikita zaidi katika majiundo ya maisha ya kiutu na Kikristo miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, akauwawa kikatili kunako mwaka 1792 wakati wa Mapinduzi ya Ufaransa. Josè Sànchez de Riò, mlei na shahidi kutoka Mexico ni kijana aliyesimama kidete kuungama na kushuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake, huku akitiwa shime na mama yake mzazi, akauwawa kikatili kunako mwaka 1828. Hawa ni mashuhuda wa imani wanaoendelea kujitokeza hata katika ulimwengu mamboleo.

Josè Gabriel del Rosario Brochero, kutoka Argentina ni mtakatifu msomi aliyeichambua Biblia “kama karanga”, akabahatika kuwamegea na kuwashirikisha watu wa Mungu utajiri wa Maandiko Matakatifu katika lugha ya kawaida kabisa iliyogusa akili na nyoyo za watu, waliotubu na kumwongokea Mungu. Alishiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa njia ya mafungo ya maisha ya kiroho, bwawa la kuosha roho za waamini; shule ya fadhila za Kikristo na kifo cha vilema na udhaifu wa kibinadamu.

Kwa njia ya mafungo ya kiroho, alibahatika kuwasha moto wa Maandiko Matakatifu katika maisha ya watu ili kupambana na changamoto za maisha kwa njia ya Mwanga wa Neno la Mungu. Ni mtakatifu aliyehubiri, akawaongoza watu, akafundisha kwa ari na moyo mkuu, huku akiwakirimia vijana wa kizazi kipya utajiri wa maisha ya kiroho. Ni mwamini aliyesimamia haki, amani na mshikamano kati ya watu; akawa ni mfano bora wa kushukuru kwa ukarimu anaotendewa na watu.

Mtakatifu Manuel Gonzàlez Garcìa ni Askofu aliyekita maisha yake katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na huko akajichotea neema na baraka ya kutenda mema na kuwaongoa wakosefu. Alipenda kufufua Ibada ya Ekaristi takatifu katika Makanisa yaliyokuwa yametelekezwa kwa sababu mbali mbali, ili kuonesha kwamba, Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Aliwahamasisha waamini kujisadaka kwa ajili ya kuwasaidia maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.

Sr. Elizabeth Catez wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, ni kisima cha utajiri wa tafakari kuhusu Fumbo la Utatu Mtakatifu, kiini cha imani na maisha ya Kikristo, changamoto na mwaliko wa kutunza ile neema ya Utakaso ambayo waamini wamekirimiwa na Mama Kanisa walipobatizwa.

Watakatifu Alfonso Maria Fusco na Ludovico Pavoni ni waanzilishi wa Mashirika ya kitawa, waliobahatika kusoma alama za nyakati wakajitahidi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya watoto, vijana na maskini; wakawasaidia katika shida na mahangaiko yao ya ndani. Kardinali Angelo Amato anahitimisha kwa kusema, hawa ndio watakatifu ambao Mama Kanisa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anapenda kuwaweka mbele ya familia kama majembe na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.