2016-10-16 14:13:00

Papa Francisko kutembelea Jimbo kuu la Milano 2017


Kardinali Angelo Scola, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano, Italia kwa niaba ya familia ya Mungu Jimboni humo anasema, wamepokea kwa mikono miwili na kwa moyo mkunjufu kabisa taarifa ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Jimboni humo, Jumamosi, tarehe 25 Machi 2017. Hiki ni kielelezo makini kwamba, Baba Mtakatifu anathamini Jimbo kuu la Milano pamoja na Mkoa mzima wa Lombardia, ambao uko Kaskazini mwa Italia. Tangu sasa, familia ya Mungu Jimbo kuu la Milano inaanza maandalizi mara moja, kwa kuunda tume maalum itakayosimamia na kuratibu hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Jimboni humo.

Akizungumza na watumishi wa Altareni zaidi ya 5000 wa Jimbo kuu la Milano, Kardinali Scola amesema, anatumaini kukutana nao tena kwa wingi namna hii wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko atakapowatembelea Jimboni humo hapo mwakani. Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kutembelea na kuzungumza na wafungwa wa gereza moja huko Milano na kama kawaida, atatembelea maeneo yaliyoko pembezoni mwa mji wa Milano, maarufu kwa shughuli za kiuchumi na kibiashara, ili kuwatangazia wenyeji wa vitongoji hivi Injili ya furaha, imani na matumaini kwa Kristo Yesu! Haya ndiyo mawazo elekezi kwa ajili ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Jimbo kuu la Milano, nchini Italia kwa Mwaka 2017. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itaendelea kukujuza yale yatakayokuwa yanajiri wakati wa maandalizi na hatimaye, hija yenyewe kwa wakati muafaka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.