2016-10-15 07:00:00

Padre Arturo Sosa achaguliwa kuwa mkuu wa Shirika la Wayesuit


Wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika la Wayesuit wamemchagua Mheshimiwa Padre Arturo Sosa Abascal kutoka Venezuela kuwa mkuu mpya wa thelathini wa Shirika la Watesuit lenye makao yake makuu mjini Roma. Padre Artusro Sosa alizaliwa kunako mwaka 1948, akajiunga na Shirika la Wayesuit kunako mwaka 1966 na kupewa Daraja Takatifu la Upadre mwaka 1977.

Padre Arturo Sosa anachukua nafasi ya uongozi kutoka kwa Padre Adolfo Nicolàs ambaye ameng’atuka madarakani rasmi hapo tarehe 3 Oktoba 2016 kutokana na umri kuwa mkubwa. Kabla ya kuchaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu uliokuwa unaendeshwa hapa mjini Roma, Padre Arturo Sosa Abascal alikuwa ni mwalikishi wa wakuu wa kanda wa Shirika la Wayesuit mjini Roma. Kati ya mwaka 1996 na mwaka 2004 alikuwa ni mkuu wa Shirika la Wayesuit kanda ya Venezuela na amewahi kuwa ni mratibu wa shughuli za kijamii na mkuu wa kituo cha utafiti cha Wayesuit, Amerika ya Kusini huko Gumila.

Kwa muda mrefu alijisadaka kwa ajili ya kuwafunda vijana wa kizazi kipya katika masuala ya elimu, kumbe, kimsingi Padre Arturo Sosa ni Jaalimu aliyebobea katika masuala ya elimu. Ni mwandishi mahiri sana wa vitabu hasa kuhusiana na historia na siasa ya maisha ya familia ya Mungu nchini Venezuela. Katika mkutano mkuu wa 35 wa Wayesuit uliofanyika kunako mwaka 2008, Padre Nicolàs alikuwa amemteua kuwa mshauri mkuu na kunako mwaka 2014 akateuliwa kuwa ni kati ya washauri wakuu wa Shirika la Wayesuit.

Taarifa inaonesha kwamba, wajumbe 212 kutoka katika nchi 66 kuanzia tarehe 2 Oktoba 2016 walikuwa wakifanya mkutano wao mkuu, kipindi cha wajumbe kukutana kwa faragha na kubadilishana mawazo; muda wa sala na tafakari na hatimaye, mapendekezo ya majina ya wale wanaotarajiwa kushika nafasi ya uongozi wa Shirika ili kuendeleza karama na utume wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola kwa Kanisa la Kristo.

Wayesuit, Jumapili tarehe 16 Oktoba 2016 wanaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kufanikisha zoezi hili la uchaguzi na baadaye wataendelea kuwachagua washauri wakuu wa Shirika pamoja na kuweka sera na mikakati ya uongozi mpya. Lakini, ikumbukwe kwamba, Shirika la Wayesuit lina nadhiri ya nne ambayo ni utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kumbe, kabla ya kuendelea na shughuli nyingine baada ya Padre Arturo Sosa Abascal kuchagulia, Baba Mtakatifu Francisko alipewa taarifa na mchakato wa uchaguzi mkuu ukaendelea kadiri ya sheria na kanuni za Wayesuit!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.