2016-10-15 09:15:00

Mwenyeheri Paulo VI: Haki, Amani na Maendeleo endelevu!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Ijumaa tarehe 14 Oktoba 2016 ameshiriki katika kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Baraza hili, ambalo katiba yake ilipitishwa na Mwenyeheri Paulo VI. Utangulizi wa kongamano hili umetolewa na Kardinali Ricardo Blazquez Perez, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania. Kongamano hili la kimataifa limeongozwa na kauli mbiu “Paulo VI na Amani”.

Haki na amani ni kati ya mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na Mwenyeheri Paulo VI katika maisha na utume wake kam Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kunako mwaka 1964, akizungumza kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, Papa Paulo VI aliitaka Jumuiya ya Kimataifa kuachana na utamaduni wa vita na badala yake kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Aliendeleza kwa kina na mapana ujumbe wa amani uliokuwa umetolewa na mtangulizi wake Mtakatifu Yohane XXIII “Amani Duniani” “Pacem in terris” kwa kukazia: ukweli, haki, upendo na uhuru. Kunako mwaka 1968 akaanzisha Siku ya Kuombea Amani Duniani.

Tangu wakati huo anasema Kardinali Parolin, Kanisa likaamua kutoka kifua mbele katika hali ya unyenyekevu ili kukabiliana na changamoto mamboleo, daima likitoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma ya binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Ni kiongozi aliyependa kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu, kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Haki, amani, maendeleo na upenso kwa maskini vikapewa msukumo wa pekee katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Mwenyeheri Paulo VI alionesha ujasiri wa pekee kwa kutembelea India kunako mwaka 1967 na huko watu millioni nne wakampokea na kumkaribisha kati yao naye akaonesha mwelekeo wa Kanisa kwa ajili ya maskini pamoja na maskini, ili liweze kuwapeleka mbinguni kwa Baba. Akiwa nchini India akaanzisha kampeni ya kimataifa ya kupambana na umaskini duniani. Kunako mwaka 1967 akaanzisha Baraza la Kipapa la haki na amani, ili kuonesha dhamana ya Kanisa katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Huu ukawa ni mwanzo wa majadiliano katika ukweli, uwazi, upendo na mshikamano na matokeo yake ni Waraka wake wa kitume “Maendeleo ya watu” “Populum Progressio”, tema iliyoendelezwa na Yohane Paulo II kwa kukazia masuala jamii na Papa Mstaafu Benedikto XVI aliyejielekeza zaidi kwa ukweli katika upendo. Amani ikawa ni jina jipya la maendeleo endelevu ya binadamu dhidi ya baa la njaa, ukosefu wa haki msingi za binadamu na vita kwa kuamini kwamba hakuna maendeleo ya kweli bila amani ya kudumu. Hiki ni kipindi cha vita baridi iliyogawa Jumuiya ya Kimataifa katika makundi. Mwenyeheri Paulo VI akajitokeza kuwa chombo na shuhuda wa upatanishi kati ya watu, akaridhia mchakato wa kuanzishwa kwa Umoja wa Ulaya kama njia ya kujenga na kudumisha amani duniani na kwamba, Jumuiya ya Ulaya ingepaswa kujenga msingi wa utamaduni wa amani kwa kutambua majanga yaliyojitokeza wakati wa Vita kuu ya Pili ya Dunia.

Kunako mwaka 1975, Vatican ikashiriki katika mkutano wa Usalama Barani Ulaya huko Helsinki ili kuweka mikakati ya amani ya kudumu Barani Ulaya na huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa ujenzi wa ushirikiano kati ya Kanisa na Nchi za Kikomunisti Barani Ulaya. Cheche za ushirikiano kati ya Kaskazini na Kusini mwa dunia zikaanza kujitokeza. Utunzaji bora wa mazingira ni mambo ambayo Mwenyeheri Paulo VI aliyagusia kwa kuona kwamba, baa la njaa, vita na ukosefu wa maji safi na salama ni mambo yaliyokuwa yanatishia Injili ya uhai. Mgogoro wa uchimbaji wa mafuta ulikuwa pia ni tishio la maisha kama ilivyokuwa pia kwa sera zilizokuwa zinakumbatia utamaduni wa kifo kwa kujikita katika ukabila, udini, utoaji mimba na mateso kwa watu. 

Mapambano dhidi ya utamaduni wa kifo yalipata chimbuko lake katika mchakato mzima wa Uinjilishaji uliopania pamoja na mambo mengine, kuwakirimia binadamu furaha ya Injili, kwa kutambua kwamba, ulimwengu mamboleo unawahitaji Wainjilishaji wanaoweza kuwatangazia watu wa mataifa furaha ya Injili kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Uinjilishaji unaojikita katika mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili hasa katika mapambano dhidi ya umaskini, njaa na ujinga, maadui wakuu wa binadamu. Uinjilishaji ulipaswa pia kujikita katika utamadunisho, ili kweli Injili ya Kristo iweze kukaa katika akili na nyoyo za waamini bila kusahau majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho. Uinjilishaji ulipania kutoa mwamko kwa waamini kushiriki kikamilifu katika masuala ya kisiasa kwa kukazia Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayojikita katika utu, heshima, haki, ustawi na maendeleo ya binadamu wote.

Kardinali Parolin anakaza kusema, Injili haiwezi kufungamana na utamaduni wa watu fulani tu, kwani amani ya kweli inapata chimbuko lake katika Kristo Yesu, kiini cha Habari Njema ya Wokovu. Uinjilishaji ulipania pamoja na mambo mengine kupambana na umaskini, ujinga, maradhi, ukosefu wa haki msingi za binadamu, ili kweli mwanadamu aweze kupata amani, furaha na matumaini katika hija ya maisha yake.

Kardinali Parolin anawakumbusha hayo wajumbe wa kongamano la kimataifa kuhusu mchango wa Paulo VI na Amani Duniani kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania. Mwenyeheri Paulo VI alitaka Injili isaidie kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.