2016-10-14 14:21:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Chakula Duniani 2016


Jumuiya ya Kimataifa tarehe 14 Oktoba 2016 imeanza rasmi maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2016 yanayoongozwa na kauli mbiu “Hali ya hewa inabadilika. Hata chakula na kilimo” yatakayofikia kilele chake hapo tarehe 16 Oktoba 2016 kwa semina na makongamano mbali mbali yanayowashirikisha viongozi wakuu na wajumbe wa Mashirika ya Chakula na Kilimo ya Umoja wa Mataifa mjini Roma. Katika maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe wake ambao umesomwa na Monsinyo Fernando Chica Arellano, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Mashirika ya Chakula na Kilimo ya Umoja wa Mataifa yaani: FAO, IFAD na WFP.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake aliomwandikia Professa Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, kwa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa mwaka 2016 anauliza swali la msingi kuhusu mambo yaliyosababisha mabadiliko makubwa ya tabianchi na athari zake katika masuala ya kilimo na chakula duniani! Je, ni watu kiasi gani wanaojihusisha na shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi duniani wanaoathirika kutokana na mabadiliko ya tabianchi? Mwishoni, Baba Mtakatifu anatoa ushauri wa mambo msingi yanayopaswa kufanyika ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi duniani yanayoendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, shughuli za binadamu kwa kiasi kikubwa zimechangia uharibifu wa mazingira na matokeo yake ni athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi changamoto na mwaliko wa kutumia vyema tafiti za kisayansi na kitamaduni katika kukabiliana vyema na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Kanuni maadili na sera bora sanjari na mabadiliko makubwa ya mtindo wa maisha ni mambo msingi katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira. Sera na mikakati inayobainishwa na Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutekelezwa kikamilifu kitaifa na kimataifa kwa kujikita katika udugu unaojenga msingi wa mshikamano wa kimataifa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wakulima, wafugaji na wavuvi ni watu wanaokabiliwa na changamoto kubwa za mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo inachangia pia mabadiliko hata katika mtindo wa maisha yao, kiasi cha kujiona kwamba, wamesahaulika na kutelekezwa na Serikali pamoja na taasisi husika. Inasikitisha kuona kwamba, ongezeko la idadi ya watu duniani linachochea tamaa ya watu kutaka kujipatia faida kubwa kwa makampuni makubwa pamoja na watu binafsi kufanya mabadiliko makubwa katika mazao na misimu yake hata wakati mwingine kwenda kinyume kabisa cha asili ya mazao haya.

Ubora wa mazao yanayozalishwa kwenye maabara una faida na hasara zake, kumbe kuna haja ya kulinda, kutunza na kuendeleza sera ya utunzaji bora wa mazingira, ili kweli chakula kinachozalishwa kiweze kutosheleza mahitaji ya ongezeko la idadi ya watu duniani badala ya maendeleo ya teknolojia ya sasa katika masuala ya chakula na kilimo kuendelea kusababisha watu zaidi ya millioni 800 kuteseka kwa baa la njaa duniani. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna idadi kubwa ya watu wanaoathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kwamba, idadi hii inatarajiwa kuongezeka maradufu, changamoto kwa watu wote kushikamana ili kulinda, kutetea na kudumisha utu na haki msingi za binadamu.

Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kuwa na ugavi sawa wa chakula duniani na kuhakikisha kwamba, chakula kinachozalishwa ni kwa ajili ya matumizi ya binadamu na wala si vinginevyo pamoja na kudhibiti uharibifu wa chakula wakati kuna mamillioni ya watu wanaokufa kwa baa la njaa duniani. Baba Mtakatifu anawataka wadau mbali mbali katika sekta ya chakula na kilimo kuhakikisha kwamba, wanashirikiana ili kujenga mfumo mpya wa Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, jambo ambalo linawezekana kabisa!

Hapa jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inajizatiti kwa ajili ya kutosheleza mahitaji ya binadamu: kiroho na kimwili. Watu wana haki ya kupata lishe bora na ya kutosha kadiri ya mahitaji yao. Mkutano wa Marrakesh kuhusu mabadiliko ya tabianchi iwe ni fursa ya kujifunga kibwebwe kutekeleza dhamana hii kwa ajili ya mahitaji ya binadamu wote sanjari na kuendelea kutekeleza Itifaki ya makubaliano ya mkutano wa mabadiliko ya tabianchi huko Paris, Ufaransa kwa kujikita katika ujasiri unaopania kuleta mwelekeo mpya wa utekelezaji wa sera za kiuchumi kielelezo makini cha utawala bora wa kitaifa na kimataifa.

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni anasema, hii ndiyo tafakari yake ambayo anapenda kuwashirikisha viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wakati huu wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa mwaka 2016, huku akiwa anawakumbatia moyoni mwake, waathirika wa mabadiliko ya tabianchi ambao wengi wao wanatoka katika Jumuiya maskini kabisa duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.