2016-10-14 16:00:00

Jubilei ya vijana wa zamani! Yaani we acha tu!


Zaidi ya vijana wa zamani wapatao 7,000 siku ya Jumamosi watakutana na Baba Mtakatifu Francisko kama  sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya wazee duniani, ili kuonesha dhamana n anafasi ya wazee katika maisha na utume wa Kanisa, bila kusahau mchango wao katika masuala ya kiimani, kijamii na kitamaduni, kwani hawa ni watu ambao wana utajiri mkubwa wa imani, maadili, ut una utamaduni ambao unapaswa kurithishwa kwa vijana wa kizazi kipya.

Vijana wa zamani wanao mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya jamii, ikiwa kama watapewa nafasi ya kushirikisha ndoto yao kwa vijana wa kizazi! Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anaendelea kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutoa kipaumbele cha pekee kwa wazee katika majiundo ya maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu kwani hawa ni hazina kubwa ambayo ikitumika barabara itasaidia kwa kiasi kikubwa kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili kwa vijana wa kizazi kipya, ambao wengi wao wanaonekana kana kwamba, wamepoteza dira na mwelekeo wa maisha kwa kuzama sana katika malimwengu yanayowaachia ukakasi na machungu katika safari ya maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.