2016-10-14 15:33:00

Bw. Antonio Guterres achaguliwa kuwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa!


Baraza kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa limemchagua Bwana  Antonio Manuel de Oliveira Guterres mwenye umri wa miaka 67 kuwa Katibu mkuu wa tisa wa Umoja wa Mataifa, wadhifa ambao ataanza kuutumikia hapo tarehe Mosi Januari 2017 hadi tarehe 31 Desemba 2021. Kabla ya kuchaguliwa kwake, Bwana Guterres alikuwa ni Kamishina mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa. Anachukua nafasi ya Bwana Ban Ki-Moon ambaye anamaliza muda wake wa uongozi mwishoni mwa Mwaka 2016.

Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR ni kati ya taasisi kubwa duniani ambazo zinatekeleza dhamana na utume wake katika nchi 126, likiwa na wafanyakazi 7,000 kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji walioko ugenini na wale wanaorejea katika nchi zao hata katika mazingira magumu. Katika maisha yake, Katibu mkuu mteule wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kunako Desemba 2013 alibahatika kukutana na kuzungumza kwa faragha na Baba Mtakatifu Francisko, muda mfupi tu baada ya kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa Katoliki, ili kuunga mkono juhudi za Baba Mtakatifu ambaye amekuwa mstari wa mbele kuwatetea wakimbizi na wahamiaji ambao kwa sasa wanaonekana kuwa kama tishio kwa maisha, usalama na mafungamano ya Jamii.

Baba Mtakatifu anapinga kabisa utamaduni wa kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine kwa kuwataka waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo na mshikamano. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican kwa wakati huo, Bwana Guterres alilipongeza Kanisa Katoliki kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa ajili ya huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa kuhakikisha kwamba, jamii inaonesha upendo na ukarimu kwa kuwapokea na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji katika shida na mahangaiko yao.

Itakumbukwa kwamba, safari ya kwanza kabisa ya Baba Mtakatifu Francisko kutoka nje ya mji wa Vatican alikwenda kutembelea Kisiwa cha Lampedusa ambacho kimekuwa maarufu sana duniani kwa kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Kitendo hiki cha Baba Mtakatifu kutembelea Lampedusa kilileta mwamko mpya dhidi ya vitendo vya ubaguzi wa rangi na hofu isiyokuwa na mashiko wala msingi, kwani watu wanapaswa kuvumiliana na kuheshimiana.

Wakati huo Bwana Guterres ambaye aliwahi kuwa Waziri mkuu wa Hispania alikaza kusema, shutuma dhidi ya wakimbizi na wahamiaji kwamba ni chanzo cha vitendo vya kigaidi, ukosefu wa fursa za ajira, usalama na mafungamano ya kijamii hazina msingi wowote. Baba Mtakatifu Francisko ni kielelezo cha matumaini mapya kwa wale waliokata tamaa na kuelemewa na matatizo ya kijamii. Ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kudhibiti mambo yote yanayosababisha vita, kinzani na migogoro ya kivita sanjari na mabadiliko ya tabianchi. Jumuiya ya Kimataifa ikidhibiti vitendo hivi, bila shaka wimbi la wakimbizi duniani linaweza kupungua kwa kiasi kikubwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.