2016-10-13 13:59:00

Utambulisho wa Umoja wa Ulaya unajikita katika msingi wa Ukristo!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hotuba yake kwenye Chuo kikuu cha Kikatoliki cha Lisbon, Ureno, Jumatano tarehe 12 Oktoba 2016 amewakumbusha wasomi na wanazuoni kwamba, misingi ya utamaduni wa Ulaya ni dawa tosha kabisa dhidi ya wasi wasi wa utambulisho wa wananchi wa Jumuiya ya Ulaya. Bara la Ulaya lina historia na utambulisho wake unaovuka mipaka ya kijiografia na lugha za wananchi wake na kwamba, mambo haya yanasimikwa katika uhuru.

Ukristo anaendelea kusema Kardinali Parolin, umechangia kwa kiasi kikubwa utambulisho wa Bara la Ulaya hata katika tofauti zake na utambulisho wake maalum. Athari za Vita kuu ya Pili ya Dunia ilikuwa ni changamoto kubwa kwa Bara la Ulaya, kuanza upya kutoka kwenye magofu ya vita hiyo, dhamana iliyotokelezwa na waasisi wa Umoja wa Ulaya kama akina: Konrad Adenauer, Robert Schuman, Alcide De Gasperi. Jumuiya ya Ulaya ikajengeka katika misingi ya watu na nchi zao, ambao hapo awali walipimana nguvu kwa njia ya mtutu wa bunduki!

Kumekuwepo na mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na Umoja wa Ulaya, ingawa hatima ya Umoja wa Ulaya kwa sasa bado iko mashakani kutokana na changamoto nyingi zinazoendelea kujitokeza kwa wakati. Jumuiya ya Ulaya imefanikiwa kuwa na sarafu moja na utambulisho mmoja wa raia wake. Mtikisiko wa uchumi kimataifa, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha Barani Ulaya pamoja na vita inayoendelea kusababisha majanga kwa watu na mali zao ndani na nje ya nchi za Ulaya ni changamoto ambazo zinapaswa kuvaliwa njuga na Umoja wa Ulaya.

Kardinali Parolin anakaza kusema, bado kuna changamoto za kijamii ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Ulaya; Idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa Barani Ulaya kutokana na kuwa na sera tenge kuhusu maisha ya ndoa na familia; ukanimungu na utupu wa maisha ya kiroho; usalama pamoja na vitendo vya kigaidi; demokrasia na uhuru wa nchi wanachama unaotishia baadhi ya nchi kutaka kujitenga na Umoja wa Ulaya kama ilivyotokea kwa Uingereza.

Zote hizi ni changamoto ambazo zinaendelea kuugawa Umoja wa Ulaya kiasi cha kushindwa kuonesha umoja na mshikamano wa dhati. Baadhi ya nchi zimekuwa zikitoa kipaumbele cha pekee kwa masilahi ya kitaifa hali inayodhohofisha umoja na mshikamano! Umoja wa Ulaya umeshindwa kutoa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa ujenzi na udumishaji wa amani ndani na nje ya Bara la Ulaya na matokeo yake, biashara haramu ya silaha inaendelea kushamiri na watu wanapoteza maisha yao.

Mashambulizi ya kigaidi ndani na nje ya Umoja wa Ulaya yamekuwa ni tishio la amani, usalama na mafungamano ya kijamii, changamoto kwa Jumuiya ya Ulaya kurejea tena kwenye misingi yake ya kitamaduni ili kujenga utambulisho wenye nguvu na mashiko! Udhaifu huu unajionesha hata katika masuala ya maisha ya kiroho na kijamii na matokeo yake ni misimamo mikali ya kidini na kiimani mambo ambayo yanagumisha majadiliano ya kidini, kiekumene na hata kijamii. Jumuiya ya Ulaya inapaswa kujizatiti ili kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Afrika ya Kaskazini na huko Mashariki ya Kati.

Kuna umati mkubwa wa watu wanaokimbia: vita, njaa, umaskini, magonjwa, majanga na ukosefu wa fursa za ajira. Nchi wanachama wa Jumuiya ya Ulaya zinapaswa kukubaliana na sera kuhusu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji sanjari na kushuhughulikia wasi wasi na hofu inayooneshwa na wananchi wa Ulaya. Yote haya anasema Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican yanawezekana ikiwa kama Umoja wa Ulaya utarejea tena kwenye misingi yake ya awali yaani Ukristo ambao umebeba historia nzima ya ukuaji wa Umoja wa Ulaya, ili kuweza kuwajibika barabara, Wakristo wakiwa mstari wa mbele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.