2016-10-13 06:41:00

Sitisheni vita nchini Syria ili kuokoa maisha ya watu!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 12 Oktoba 2016, kwa mara nyingine tena ameonesha uwepo wake wa karibu kwa waathirika wote wa vita dhidi ya ubinadamu inayoendelea huko nchini Syria. Anasema, kwa nguvu na uweza wake wote kutokana na dharura iliyopo kwa sasa wahusika wote wa mgogoro huu kusitisha vita mara moja ili walau kutoa nafasi ya kuwasaidia wananchi,na hasa zaidi watoto ambao wanaendelea kuteseka kutokana na mashambulizi ambayo ni kinyume kabisa cha utu wa binadamu.

Baba Mtakatifu pia amekumbusha kwamba, Alhamisi tarehe 13 Oktoba 2016, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kupambana na Athari za Majanga asilia, ambayo kwa mwaka 2016 yanaongozwa na kauli mbiu “Kupunguza vifo”. Majanga asilia yanaweza kuepukika au kupunguzwa kwa kiasi kikubwa kwani sehemu kubwa ya majanga haya ni kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na binadamu.

Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuunganisha nguvu zake zote kwa ajili ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawataka watu kujenga utamaduni wa kuzuia majanga asilia kwa kutumia msaada unaotolewa na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwani waathirika wakubwa wa majanga asilia ni Jumuiya za watu maskini duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.