2016-10-13 15:26:00

Papa: Mkristo wa kweli daima hutafuta msamaha wa Mungu na kutenda mema


Mkristo wa kweli daima hutambua msamaha wa Mungu  kila siku anapoendelea kutembea katika   njia ya kuelekea  kukutana na Mungu.  Baba Mtakatifu Francisko  aliasa Alhamisi hii mapema  asubuhi , wakati akiongoza Ibada ya Misa katika Kikanisa cha Mtakatifu Marta, ndani ya Vatican. Baba Mtakatifu alizungumzia  umbile la Mkristo mzuri , akitaja kwamba ni yule ambaye daima anajisikia kubarakiwa Bwana, katika kutenda mema. Na mwenye kusadiki kwamba baraka hizo zinatoka kwa  Baba ambaye ni Mungu mwenyewe.

Homilia ya Papa Francisko, ilitafakari somo kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa  Waefeso, ambamo mna maelezo juu ya sifa ya baraka hii ,akisema  kwamba  kuwa Mkristo ni kuwa mtu wa Mungu,  kwa kuwa Mungu,  humchagua yule anayempenda  kwa kumwita kama mtu binafsi na kumpa jina.  Kumbe Mungu hawaiti watu katika ujumla wao kama kundi la watu  lakini humwika mmojammoja  kama anavyopenda , kumbe basi walioitwa wanakuwa ni  wateule wa Baba.

Baba Mtakatifu alieleza na kutaja fuaraha ya Mungu katika kuchagua wateule wake , akiifaninsha furaha hiyo na wanandoa wanaotarajia kupata mtoto, jinsi wanavyoifurahia siku hiyo ya mtoto kuzaliwa katika familia yao ,  na ndivyo ilivyokuwa kwa MUngu , anavyofurahia kumwita mtu kwa jina lake na kumeingiza katika framilia yake, akiwa tayari kutoa kila ulinzi kwa ajili ya  usalama mkubwa wa wateule wake. Papa alieleza na kusisitiza kwamba Mungu Baba amemchagua kila mtu mmoja mmoja na si kama kundi la watu. Na hili ni msingi wa uhusiano wa Mungu na wateule wake. Na hivyo tunaweza sema kwamba, Mungu  Baba anatupenda, alituchagua na kumpa jina kila mmoja.

Pia aliendelea kufafanua kwamba,  Mkristo asiyekuwa na hisia kwamba amechaguliwa yeye binafsi na Baba, ila kama kundi, basi imani ya Mkristo si ya kweli ,  bali ukristo wake ni sawa na kujiunga katika  ushabiki wa  vyama au timu za michezo.

Lakini kwa mwenye  kutambua  kwamba yeye ni mteule wa Mungu ,anakuwa ni  Mkristo wa kweli, na huona haja ya kupata msamaha wa Mungu kwa mapungufu yake, yanayotaka kuchafua hadhi ya mahusiano yake kama mteule wa  Mungu.  Papa aliongeza kwamba, kwa kuishi na hisia hizi,  moyo wa Mkristo mteule hujazwa na faraja kubwa, kwamba Mungu hawezi kumtelekeza.  Papa pia alizungumzia pia sehemu ya pili ya baraka za Mkristo katika hisia za kusamehewa , iwe kwa mwanamume au mwanamke, akisema kwamba,  Mkristo asiyejisikia amesamehewa  na Mungu , basi huyo si Mkristo wa kweli.  

Papa aliendelea kutaja sehemu ya tatu katika hili akisema kwamba, Mkristo iwe mwanamume au  mwanamke anayetembea kuelekea ukamilifu katika njia yake ya maisha ni lazima akutane na  Kristo aliyemkomboa. Hivyo maisha ya Kikristo ni mwendelezo wa hija ya maisha, daima ikiwa ni kupiga hatua  mbele na Kristo katika njia ya maisha ya kila siku, bila kusitishwa na hofu ya maisha, au  hofu ya kifo, hofu ya bosi, au mambo mengine  hata yale ya kutisha sana.  Ni lazima Mkristo safi , aendelee na dafari hii ya maisha kama mteule wa Mungu katika hali ya utulivu  na matumaini kamili,  kwa kuwa anajua mahali anapokwenda. Ni lazima kwa na utambuzi kwamba , Ukristo ni safari ya maisha, inayoandamana daima kutenda mema bila kuchoka au kuw ana ukomo.  

Papa alihitimisha homilía yake, kwa kutoa mwaliko kwa kila Mkristo, kukubali kuongozwa na utambulisho wa Kikristo, uliotajwa katika Injili ya heri, heri wenye moyo safi maana watamwona Mungu , kwa  sababu wao ni mteule  na kwa sababu wanatambua msamaha wa Mungu katika njia yao ya maisha. Na kwa utambuzi kwamba, kila mmoja akiwa ameitwa kwa  jina lake katika ubatizo, anapaswa kuomba  msamaha wa Mungu, kama baraka kutoka kwa  Bwana na utambulisho wa Mkristo.








All the contents on this site are copyrighted ©.