2016-10-13 13:36:00

Mchango wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza: Uekumene, amani na mazingira!


Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, ameandika kitabu kama kumbu kumbu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Upatriaki huu. Papa mstaafu Benedikto XVI pamoja na Baba Mtakatifu Francisko wameshiriki katika kuandika utangulizi wa kitabu hiki, kinachoonesha hija ya pamoja katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene baina ya Makanisa haya mawili.

Kitabu hiki kinachojulikana kama “Bartholomew Apostle and Visionary” kinamwonesha Patriaki Bartolomeo wa kwanza kuwa kweli ni mtume na kiongozi mwenye maono. Papa mstaafu Benedikto XVI anamwelezea kuwa ni mwenza katika hija ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kiongozi ambaye anaendelea kujipambanua katika kupigania haki, amani, umoja na maridhiano kati ya watu wa dini mbali mbali. Ni kiongozi ambaye amejipambanua katika kusimama kidete kulinda na kutetea utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Katika utangulizi wake, Baba Mtakatifu Francisko anampongeza Patriaki Bartolomeo wa kwanza wakati huu anapoadhimisha Jubilei ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Upatriaki wa Costantinopoli. Anamkumbuka kwa namna ya pekee, tangu siku ile alipokuwa anaanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kunako mwaka 2013, tangu siku ile akajisikia moyoni mwake kwamba, alikuwa kweli amekutana na kiongozi aliyekuwa anatembea katika njia ya imani inayojikita katika Mapokeo ya Kiorthodox.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, amebahatika kukutana, kuzungumza na kusali pamoja na Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwa nyakati mbali mbali, matukio ambayo yameimarisha umoja na udugu kati ya viongozi hawa wawili wenye dhamana pevu ya shughuli za kichungaji hasa katika kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika maisha ya watu: kiroho na kimwili. Wameendelea kuimarisha umoja na mshikamano unaofumbatwa kutoka katika udugu wa akina Mtakatifu Petro na Andrea, nguzo kuu kwa Makanisa haya mawili; Mitume ambao waliyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, watangulizi wao yaani Mwenyeheri Paulo VI na Patriaki Athenagora, takribani miaka hamsini iliyopita, walianzisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene kwa kutaka kujenga na kuimarisha umoja wa Kanisa; kwa kuganga na kuponya madonda ya utengano, ili kuweza kuwa na umoja katika imani na mapendo, kama ilivyokuwa wakati wa Kanisa la mwanzo. Leo hii viongozi hawa kama ndugu katika imani wanapenda kujizatiti ili kujenga umoja wa Kanisa kwa ajili ya wokovu wa wengi, haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati.

Kama viongozi wa Kanisa anaendelea kufafanua Baba Mtakatifu Francisko, wanao wajibu shirikishi unaobubujika kutoka katika Habari Njema ya Wokovu unaowataka kusimama kidete ili kujenga ulimwengu unaosimikwa katika misingi ya utu na heshima ya binadamu sanjari na uhuru wa kuabudu. Wanao wajibu wa kuhamasisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anampongeza na kumshukuru Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwa mchango na tafakari zake za kina kuhusu mazingira. Ni kiongozi anayeguswa na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia kutokana na vita, ubaguzi na vitendo vya kikatili dhidi ya ubinadamu; mambo yanayoonekana kana kwamba, yanazidi kuongezeka kila kukicha! Ni wajibu wao wa kimaadili kuhakikisha kwamba wanasaidia mchakato wa ujenzi wa wa utamaduni wa upendo na mshikamano, ili kukuza na kudumisha hija ya haki, amani na upatanisho katika ukweli na uwazi sanjari na ujenzi wa umoja wa Kanisa, ili kwa pamoja Wakristo waweze kutangaza na kushuhudia Injili ya amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu.

Kutokana na mchango huu anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko ndiyo maana anaungana na watu wote wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, Patriaki Bartolomeo wa kwanza anapoadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Upatriaki wa Cotsntinopoli.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI anasema, katika utangulizi wake kwenye kitabu hiki kwamba, kweli Patriaki Bartolomeo wa kwanza ni kiongozi wa watu, mpole na mnyenyekevu, mwenye utajiri mkubwa wa lugha inayomwezesha kuwasiliana na watu mbali mbali kwa urahisi zaidi. Ni kiongozi mwenye imani thabiti kwa Kristo na Kanisa lake; Kristo ambaye ni ukweli, njia na uzima anayepaswa kutangazwa na kushuhudiwa na wote. Ni kiongozi anayepania kujenga utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana, ili wote waweze kumwendea na hatimaye, kukutana na Kristo Yesu, wakiwa wameungana na kushikamana. Ni kiongozi anayepania ustawi na mafao ya wengi; utunzaji wa mazingira kama sehemu ya kazi ya uumbaji.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anapenda kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu; umoja wa Wakristo; dhamana anayoitekeleza katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI anamshukuru na kumpongeza Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwa kumtembelea katika makazi yake mapya, ili kuonesha uwepo wake wa karibu na kwamba, makazi haya mapya yanapambwa na zawadi mbali mbali alizopokea kutoka kwake, kielelezo makini cha mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha. Anamaliza kwa kumtakia kheri na fanaka katika maisha na utume wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.