Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake kwa mahujaji na wageni, ametoa mwaliko kwa watu wote kila siku kukumbuka akilini, fadhila na utendaji wa watu watakatifu kwa mfano Mama Tereza wa Calcutta, ambaye anaonyesha waziwazi uso wa huruma wa Kristo , ulivyo na uwezo wa kuleta mabadiliko makubwa katika utamaduni mahalia. Mafundisho ya Papa yalilenga Injili ya Mtakatifu Mathayo, ambamo Bwana anatuambia kwamba tutahukumiwa kwa jinsi tunavyo wahurumia wengine.
Alisema kwa Jumatano hii, tukiendelea kuelekea katika kukamilika kwa Jubilee maalum ya mwaka Mtakatifu wa huruma , ambamo katika katekesi zake amekuwa akiizungumzia huruma ya Mungu inayoonekana kupitia hasa Mwana wa Mungu, na wajibu wetu, kama wafuasi wa Yesu, katika kuwa na huruma, kama Baba wa Mbinguni, pia anaendelea kuizungumzia huruma ya Mungu, kama ilivyoandikwa katika Injili ya Mathayo, ambamo Bwana anasema kwamba, tutahukumiwa kulingana na huruma tunayo mwonyesha kupitia kwa watu wanaotuzunguka ,wake kwa waume.
Papa Francisko ameeleza na kufanya rejea kwa maneno ya Yesu, alipowaambia wanafunzi wake ,” kuweni na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma” (Lk 6,36). Papa anasema , maneno haya maana yake hasa yanailenga katika dhamiri na uhusiano wa kila Mkristo kwa watu wengine. Na kwamba katika ukweli wake,kuiishi huruma ya Mungu maana yake ni kuwahurumia wengine. Na wale wanaopokea huruma hii , basi wanapaswa kuwa ishara na chombo kinachoibeba huruma hiyo kwa ajili ya kuwafikishia watu wengine. Huruma hii zaidi ya yote ,si tu kwa wakati fulani fulani lakini inapaswa kumwilishwa katika maisha na utendaji wa kila siku.
Papa alieleza na kuhoji kumbe basi ni kwa namna gani tunaweza kuwa mashahidi wa huruma ya Mungu? Alijibu akisema ni vyepesi sana, kwa kuwa Bwana huionyesha njia yenyewe kwamba, si kwa matendo makubwa, lakini ni kupitia huduma ndogondogo tu katika maisha ya kawaida. Utendaji huo mdogomdogo mbele ya macho ya Bwana, huwa na thamani kubwa, kama alivyokwisha sema Yesu kwamba, tutahukumu kwa hayo. . Yesu alisema, kila tunapotoa msaada kwa watu maskini na wanyonge wasiokuwa na kitu , kama kuwapa chakula, kinywaji, mavazi au kuwatembelea wagonjwa,wafungwa na walio katika dhiki, wafiwa na kukaribisha wageni , huko ni kumhudia Yesu mwenyewe( Mt 25 -31-46).
Papa Francisko pamoja na kuzungumzia matendo haya aliyoyataja kwamba Kanisa huyaita matendo ya huruma ya kimwili, kwa kuwa ni kumsaidia mtu mhitaji kihali, pia alitaja kwamba, kuna matendo mengine saba ya huruma ambayo ni kiroho, ambayo pia ni muhimu sana hasa katika nyakati hizi za leo , kwa kuwa hugusa moyo wa mtu mwenyewe na kwa mara nyingi hutufanya kuteseka zaidi. Matendo hayo ni utoaji wa ushauri kwa wenye mashaka, kuwafundisha wasiojua, kushauriana wenye dhambi, kuwafaraji wanaoteseka, kusamehe mwenye makosa, kuwa na uvumilivu wale wanaotukosea na kuwaombea walio hai na wafu.
Papa aliendelea kusema kwamba, kwa ajili ya kuonyesha imani hai, hayo yote na yafanyike kimyakimya bila mbwembwe,ila kama utendaji wa kawaida. Alieleza na kutoa mwaliko kwa watu wote kuyaishi hayo kwa kutazama mfano wa maisha ya Watakatifu kama vile Mama Teresa wa Calcutta, alivyo ionyesha na kuitangaza sura yenye huruma ya Kristo, inayoweza kubadili utamaduni wa wale walio karibu nasi. . Papa aliomba daima na tuweke akilini mwetu haya huku tukijitahidi kuyaishi katika utendaji wa kila siku kimya kimya.
Baada ya Katiekesi kama kawaida Papa alisalimu makundi mabalimbali yaliyofika kwa wingi kusikiliza kateksi yake , ambamo Jumatano kwa wale waozungumza Kiingereza, Afrika wengi walitoka Ghana, Namibia na Nigeria. Kwao wote aliwatakia Jubilee njema ya Mwaka wa Huruma , iweze kuwapa neema ya kufanya mabadiliko ya kweli kiroho, kwao wenyewe na kwa familia zao, pia akimtakia kila mmoja wao furaha na amani katika Bwana wetu Yesu Kristo.
All the contents on this site are copyrighted ©. |