2016-10-12 11:04:00

Baraza la Makardinali 19 Novemba 2016


Makardinali Wapya 17 walioteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kufunga maadhimisho ya Jubilei ya Bikira Maria, kati yao 13 wanayo haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na wengine 4 wamekwisha kupoteza haki hii kutokana na umri wao kuwa mkubwa zaidi. Baba Mtakatifu anapenda kuona Baraza la Makardinali likiwa na sura ya Ukatoliki kwa kuwa na wawakilishi kutoka sehemu mbali mbali za dunia na wala si kutoka katika sehemu moja tu ya dunia.

Makardinali wateule ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na mashuhuda amini wa Kristo na Kanisa hasa katika maeneo tete na yenye migogoro ya muda mrefu! Uteuzi wa Padre Ernest Simon, kutoka Albania mwenye umri wa miaka 88 umewagusa watu wengi, kwani hutu ni Padre ambaye kwa muda wa miaka 28 alitumia adhabu kifungoni pamoja na kufanyishwa kazi ngumu wakati wa utawala wa Kikomunisti nchini humo. Ni Padre ambaye aliwahi kuhukumiwa mara mbili adhabu ya kifo, lakini akaokolewa na kwa huruma na neema ya Mungu!

Tarehe 19 Novemba 2016 atakuwa ni kati ya Makardinali wapya watakaosimikwa na Baba Mtakatifu Francisko katika mkesha wa kufunga maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, muda wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata huruma na upendo wa Mungu katika safari ya maisha ya Kikristo! Padre Ernest anakaza kusema, licha ya kuteuliwa kuwa Kardinali ataendelea kushikamana na familia ya Mungu nchini Albania, kama shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu. Kwa namna ya pekee, anapenda kuchukua nafasi hii, kumshukuru kwa dhati kabisa Baba Mtakatifu Francisko kwa kumwona na kumteuwa kuwa Kardinali.

Takwimu zinaonesha kwamba, Mwenyeheri Paulo VI alibahatika kumteua Kardinali mmoja tu; Papa Yohane Paulo II akateuwa Makardinali 94 kati yao waliokuwa na haki ya kupiga na kupigiwa kura walikuwa 21 na wengine 73 hawakuwa na haki hiyo! Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI aliteuwa Makardinali 78 kati yao 56 wakiwa na haki ya kupiga na kupigiwa kura.

Hadi sasa Papa Francisko amekwisha kuteuwa Makardinali 55 kati yao 44 wanahaki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na wengine 11 hawana haki hii kisheria. Kwa sasa kuna Makardinali 228 kati yao 121 wana haki ya kupiga na kupigwa kura wakati ambapo Makardinali 107 hawana tena haki hii.

Makardinali kutoka Barani Afrika kwa sasa ni 24, kati yao wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura ni 15 na wengine 9 hawana haki hii tena. Takwimu zinaonesha kwamba, Bara la Ulaya ndilo linaloongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya Makardinali 112, kati yao wenye haki ya kupiga kura ni Makardinali 54. Italia ni nchi ambayo inaongoza kwa kuwa na Makardinali wengi zaidi duniani, ambao kwa sasa ni 46, ikifuatiwa na Marekani ambayo ina Makardinali 18, Brazil Makardinali 11. Nigeria inaongoza Barani Afrika kwa kuwa na Makardinali 3, kati yao mmoja tu ndiye mwenye haki na kupiga na kupigwa kura. Historia inaonesha kwamba, Papa Paulo VI ndiye aliyeweka idadi ya Makardinali 120 kushiriki katika mchakato wa kura kwa ajili ya kumpata Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwasindikiza Makardinali kwa sala katika maisha na utume wao, ili waweze kumsaidia kwa ushauri makini katika kuliongoza Kanisa la Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.